
TANZIA: Sheikh Abuu Idd afariki, Rais Samia amlilia
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Ali Mbwana, kutokana na kifo cha Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mwinyi Amani (Mnyamani), uliopo Buguruni jijini Dar es Salaam, Sheikh Muhammad Idd (Abuu Idd), kilichotokea leo Alhamisi Januari 30.
Katika taarifa yake kwa umma, Rais Samia, amemtaja Abuu Idd, ambaye pia alikuwa Mshauri wa Mufti, kuwa ni mtu aliyeipenda nchi yake, mwalimu katika imani, mlezi wa wengi katika imani, mpenda haki, mpenda ukweli, umoja, amani na utulivu wa nchi yetu, aliyetumia muda wake kuyasimamia na kufundisha hayo kupitia mawaidha yake.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Sheikh Muhammad Iddi (Abuu Iddi), Imamu Mkuu wa Msikiti wa Mwinyiamani, Mshauri wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Ali Mbwana na Mratibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, kilichotokea leo Alhamisi, Januari 30, 2025.
“Natoa salamu za pole kwa familia, Mufti Mkuu wa Tanzania, Waislamu wote nchini, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu,” ameandika Rais Samia na kuongeza:
” Tumeondokewa na mtu aliyeipenda nchi yake, mwalimu katika imani, mlezi wa wengi katika imani, mpenda haki, mpenda ukweli, umoja, amani na utulivu wa nchi yetu, aliyetumia muda wake mwingi kuyasimamia na kufundisha hayo kupitia mawaidha yake.
“Mwenyezi Mungu ampe Kauli Thabit, amsamehe makosa yake, amzidishie katika mizani mema aliyotenda, na ampe nafasi katika Pepo yake.
“Inna lillahi wa inna ilayhi raji’un,” imemaliza taarifa hiyo.