Baada ya moto Ofisi za TRA Kariakoo, huduma sasa zahamia Diamond Plaza, Mariam Tower

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imewatoa shaka Walipa Kodi wa Mkoa wa Kikodi wa Kariakoo, ikisema moto ulioteketeza Ofisi za Mamlaka hiyo Mtaa wa Kipata, hautokwamisha kuhudumia kwao na kwamba imehamishia huduma na Ofisi hizo kwa muda katika majengo ya Diamond Plaza lililopo mitaa ya Samora na Mirambo na Mariam Tower lililopo Shauri Moyo jirani na Shule ya Uhuru.

Majira ya saa 6 mchana wa leo Alhamisi Januari 30, moto ambao chanzo chake hakijajulikana, ulilipuka na kuteketeza ghorofa la nne la jengo lililopo makutano ya Kipata na Lumumba jijini Dar es Salaam, kabla ya kudhibitiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na wananchi wa maeneo ya Kariakoo waliokimbilia tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya TRA, iliyotolewa na Idara ya Mlipakodi na Mawasiliano, Mamlaka hiyo imewashukuru walioshiriki kuudhibiti moto huo, na kwamba TRA itaendelea kutoa huduma bora kwa Walipa Kodi wa Mkoa wa Kikodi wa Kariakoo katika Ofisi hizo mbili zilizo jirani na ofisi zilizoungua, huku ikisisitiza kuwa huduma zote hazitosimama zitatolewa kwa ubora sawa na wa awali kabla ya janga hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *