Simba yashindwa kurejea kileleni, ‘back pass’ ya Chasambi yaiponza

JARIBIO la Wekundu wa Msimbazi Simba kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, limekwaa kisiki baada ya dakika 90 za sare ya bao 1-1 dhidi ya Fountain Gate FC ya Manyara, mechi iliyounguruma kwenye dimba la Kwaraa, mjini Babati.

Leonel Ateba aliitanguliza Simba baada ya kufunga bao la uongozi dakika ya 57, lakini dakika 16 kabla ya filimbi ya mwisho, mtoa pasi ya bao hilo, Ladack Chasambi, alijifunga alipopiga shuti akijaribu kumrejeshea kipa wake Moussa ‘Pinpin’ Camara, ambaye alishindwa kuuzuia na kutinga kimiani.

Jitihada za Simba kupata bao ili kurejea kileleni mwa msimamo zilikutana na kigingi kizito baada ya mlinda mlango Noble John kuwa kwenye kiwango bora langoni, na hata alipotokewa kwa kadi nyekundu baada ya mbili za njano, Fountain Gate walisharejea mchezoni kufanikiwa kuvuna sare hiyo ambayo ni muhimu zaidi kwa Yanga kuliko wenyewe.

Kwa matokeo hayo, ambayo Simba watapaswa kujilaumu wenyewe, baada ya kucheza dakika tisa za nyongeza bila kumtungua mchezaji wa ndani aliyekaa langoni baada ya kipa wao kulimwa ‘red card’ wakiwa wameshamaliza ‘sub,’ wamefikisha alama 44, moja nyuma ya Mabingwa Watetezi Yanga, wote wakiwa na michezo 16.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *