ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Sheria na Wanachama wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Eliud Mvela, amesema kielelezo cha Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kutambua, kuthamini na kujali mafanikio ya Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia, ni kumpa heshima ya kugombea nafasi hiyo bila kupingwa na sio kufuta uchaguzi ujao.
Mvela, ambaye amekuwa sehemu ya uongozi wa soka tangu zama za Chama cha Soka Tanzania (FAT) ya Mwenyekiti Muhidin Ndolanga, na baadaye TFF ya Leodigar Tenga, Jamali Malinzi na kisha ya Karia, ameyasema hayo baada ya mapendekezo ya klabu za Simba na Yanga katika Mkutano Mkuu wa TFF juzi kutaka uchaguzi wa Rais mwakani, usiwepo.

Katika Mkutano Mkuu wa 19 wa TFF, uliofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro Ijumaa ya Desemba 21, Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu, aliutaka mkutano huo kupitisha azimio la pamoja la kutokuwa na Uchaguzi wa Rais mwakani, wazo lililoungwa mkono na Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said na wajumbe wengine.
Kauli ya Mvela inaendana na ufafanunuzi uliotolewa na shirikisho hilo kupitia Makamu Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, ambaye alisema njia bora ya kumbakisha Karia madarakani ni wanachama wote wa shirikisho kumwekea dhamana (endorsement) tapochukua fomu ya kuwania urais na sio kuufuta uchaguzi.
Akizungumza na Sports Extra ya Clouds FM, Mvela ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, alisema Karaia ndiye kiongozi wa juu aliyeipa mafanikio makubwa Tanzania tangu kuundwa kwa mamlaka hiyo ya soka, lakini haipaswi kufutwa kwa uchaguzi wa Rais, bali wadau wakubali kutompinga.
“Mimi naamini hoja ya msingi ni kwamba, uchaguzi uwepo, Karia apitishwe bila kupingwa katika nafasi yake, yaani kusiwe na mgombea, kwa maana ya kwamba watu wasijitokeze kuchuana naye kwa ajili ya kumpa heshima kwa kazi kubwa na nzuri aliyofanya katika vipindi viwili vya utawala wake.
“Na mimi nafikiria hivyo pia na hatokuwa mtu wa kwanza (kupita bila kupingwa), mmeona Rais CAF imetokea hivyo, Rais wa FIFA ilikuwa hivyo pia. Suala ni kuamua kutokuweka mgombea na watu wakakubaliana na hilo, waliotoa wazo hilo, nadhani wanashawishi watu wasijitokeze kugombea naye, kwani aliyepo anatosha,” alisema Mvela.
Kigogo huyo akaongeza kwamba: “Kwa maana hiyo, sio kwamba Uchaguzi wa Rais TFF ufutwe, Hapana. Wanapaswa kushauri wampe Karia heshima ya kuendelea na awamu nyingine kutokana na kazi kubwa aliyofanya, katika nafasi yake kusiwe na mgombea, hata nafasi ikitangazwa kuwepo, abaki peke yake, hiyo ni sehemu ya heshima.
“Katika hilo mimi sidhani kama kuna tatizo, na wala sio kwamba kuna uminywaji wa demokrasia, kwa sababu wakati mwingine kwenye hizi taasisi, mnaangalia tu mtu anatosha kiasi gani, mnaangalia mchango wake na mafanikio yake, nafikiri ndivyo walivyojaribu kuvizingatia kwa Karia,” alisisitiza Mvela.
“Kila mmoja hapa ni shuhuda wa mafanikio makubwa ya Karia katika uatawala wake, ni makubwa kuliko miaka yote tangu utawala wa soka nchini uanze. Mimi nilikuwepo katika uongozi wa Soka la Tanzania tangu enzi za Ndolanga, akaja Tenga, kisha Malinzi na baadaye Rais Karia,” alisema na kuongeza:
“Vipindi vyote hivyo, mimi nimekuwa sehemu ya uongozi na lazima nikiri kwamba kipindi cha uongozi wa Karia tumepata mafanikio makubwa kama taifa, na ndio maana watu wanafikia mahali pa kusema ama kupendekeza uchaguzi usiwepo. Sio kwamba usiwepo, uwepo lakini ni suala la kukaa na kukubaliana kwamba huyu tusimuwekee mgombea katika nafasi yake.”