MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillus Wambura, amefanya mabadiliko madogo kwa Wakuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani.
IGP Wambura amemhamisha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Ramadhani Ng’anzi, kutoka kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, kwenda Makao Makuu ya Upelelezi Dodoma kuwa Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Maadili ya Jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, nafasi ya Ng’azi kwa sasa inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) William Mkonda ambaye alikuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Kanda Maalum Dar es Salaam.
Pia IGP Wambura amemhamisha aliyekuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Boniphace Mbao, kutoka Dodoma kwenda kuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Kanda Maalum Dar es Salaam.
Aidha, aliyekuwa Mkuu wa Elimu kwa Umma Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Michael Deleli, amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi Dodoma kuwa Kaimu Mkuu wa Maadhimisho ya Kitaifa.
Naye Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Nassoro Sisiwaya, ambaye alikuwa Mkuu wa Operesheni Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, amehamishiwa Mkoa wa Kilimanjaro kwenda kuwa Mkuu wa Usalama Barabarani wa Mkoa huo.
