Rais Dk. Mwinyi kuzindua Maabara, Ofisi za TAEC Z’bar J’tatu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akizungumza na waandishi habari jijini Dodoma kuhusu uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Maabara ya Tume ya Nguvu za ATOMU utakaofanyika eneo la Dunga-Zuze, Zanzibar.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omari Kipanga,

DODOMA, TANZANIA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajia kuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa Jengo la Maabara na Ofisi za Kanda ya Zanzibar ya Tume ya Nguvu ya Atomu Tanzania (TAEC), utakaofanyika Jumatatu Novemba 11, huko Dunga-Zuze, visiwani Zanzibar.

Maabara na Ofisi za Kanda ya Zanzibar ya TAEC, ni zao la ushirikiano baina ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na tume hiyo, lengo likiwa ni kufikisha huduma kwa wananchi, ambapo wamejenga ofisi na maabara za nyuklia katika kanda nne.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma juzi Alhamisi Novemba 7, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, aliyezitaja kanda hizo kuwa ni Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza), pamoja na hiyo ya Zanzibar.

“Lengo la kujenga ofisi katika kanda zilizotajwa ni kusogeza huduma kwa wananchi kupitia ofisi mbalimbali za TAEC, na uzinduzi wa Maabara na Ofisi za Zanzibar utafanyika Jumatattu ya Novemba 11 kuanzia saa 5 asubuhi, mgeni rasmi akiwa ni Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi.

“Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo TAEC ilielekezwa kuhakikisha kuwa inaendelea kuimarisha huduma, tafiti na ubunifu unaolenga kuongeza wigo wa matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali nchini.

“Sambamba na hilo, hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za uthibiti na kuhamasisha matumizi salama ya nyuklia karibu na wananchi wa Zanzibar, tukiamini kwamba teknolojia ya nyuklia ikitumika vizuri, inaweza kuongeza tija katika sekta mbalimbali,” alibainisha Profesa Mkenda.

Akitolea mifano hai ya matumizi hayo, Prof. Mkenda alisema teknolojia hiyo inatumika kuchunguza na kutibu ugonjwa wa saratani, kuboresha mbegu za mazao hasa yale ambayo yana ugumu kustawi na yanatoa mazao kidogo na kuua vimelea vinavyosabisha chakula kuharibika kudhibiti kuzaliana kwa wadudu wanaoeneza magonjwa.

Alitaja matumizi mengine salama ya teknolojia hiyo kuwa ni kuhakiki uimara na ubora wa maungio ya matenki na mabomba makubwa ya mafuta au maji, kuhakiki ubora katika ujenzi wa barabara na reli, kusafisha maji taka kwa ajili ya kutumika katika shughuli za utafiti wa mafuta, gesi na kadhalika.

Aliongeza kwamba, pamoja na manufaa yaliyoainishwa, kumekuwa na ongezeko kubwa la fursa za kutumia Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia katika sekta mbalimbali nchini, kama vile kilimo, afya, viwanda, mifugo na maji na kuwa matumizi ya teknolojia yatachangia maendeleo katika nyanja hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *