Na Makuburi Ally
ALIYEKUWA Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (SHIWATA), Suleiman Kissoki amefariki usiku wa kuamkia leo nyumbani kwake Tabata jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Katibu Mkuu wa Shiwata, Michael Kagondela alisema hadi jana jioni, marehemu alikuwa ofisini Ilala Bungoni akiendelea na majukumu yake.
Kagondela alisema wanatarajia kumzika marehemu huyo kwenye makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam saa 10 jioni ambako wadau mbalimbali wakiwemo wasanii, wanamichezo na wengineo walijitokeza kumsindikiza.
Kaka wa marehemu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA), Mussa Kissoki alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu kazi yake haina makosa.
Kissoki alisema kama binaadamu yatupasa tujiandae kwa ajili ya kifo kwa sababu hatujui siku wala saa mauti yatakapotufika.
Mbali ya kuwa Makamu Mwenyekiti wa Shiwata, marehemu ametumikia nyadhifa mbalimbali ikiwemo Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA).
