KAMATI ya Kitaifa ya Mazishi ya Viongozi, imetoa ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kwanza Mstaafu na Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Cleopa David Msuya, inayoonesha mwili wake utaagwa jijini Dar es Salaam Jumapili Mei 11 na kuzikwa kijijini kwake Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro, Jumanne Mei 13.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ataongoza wakazi wa Dar es Salaam Jumapili kuaga mwili wa marehemu Msuya katika Viwanja vya Karimjee, na atazikwa Jumanne kwa Mazishi ya Kiserikali yatakayoongozwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Hayati Msuya alifariki dunia Mei 7 kwenye Hospitali ya Mzena, Dar alikokuwa akipatiwa matibabu na kutangazwa siku hiyo hiyo na Rais Samia, aliyetoa siku 7 za maombolezo zitakazoishia Mei 13, siku ambayo atazikwa kijijini kwake Usangi. Ratiba ya mazishi hayo imetangazwa leo jioni na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
“Kesho Jumamosi Mei 10, mwili wa marehemu Msuya utapelekwa nyumbani kwake Upanga jijini Dar es Salaam kwa taratibu za kifamilia, kabla ya Jumapili Mei 11, Rais Samia kuongoza Watanzania waishio Dar katika ibada ya kuuombea mwili huo katika Viwanja vya Karimjee, kuanzia saa 3 asubuhi na tunatatajia itaisha saa 7 mchana.
“Jumatatu Mei 12 mwili wa marehemu Msuya utasafirishwa kwa ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanga, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA). Baada ya kutoka KIA utasafirishwa kwa magari kwenda Uwanja wa Cleopa Msuya uliopo Mwanga, ambako viongozi wa Serikali na wananchi watapata fursa ya kuuaga kuanzia saa 5 asubuhi.
“Baada ya hapo, saa 10 ya Jumatatu hiyo hiyo mwili wa marehemu utapelekwa kijijini kwake Usangi, ambako kutakuwa na ibada fupi. Jumanne Mei 13, ndio itakuwa siku ya mazishi ya hayati Msuya, ambapo ratiba itaanza na Ibada Maalum kwenye Kanisa KKKT lililopo Usangi, kisha mazishi yatayoongozwa na JWTZ.
“Baada ya mazishi hayo kufanyika, kutakuwa na salamu za viongozi wachache, akiwemo Rais Dk. Samia na kuhitimisha shughuli za mazishi,” amebainisha Gerson Msigwa ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali wakati akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari kwenye Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika, jijini Dar es Salaam.
