Prof. Mkenda ataka ‘E-Learning Africa’ iwe chachu ya Tanzania kujipanga kimkakati

DAR ES SALAAM, TANZANIA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Aldoph Mkenda, amewataka Wadau wa Elimu nchini kulitumia vema Kongamano la Kimataifa la 18 na Maonesho ya Elimu ya Kidijitali (E-Learning Afrika), ili kuendana na kasi ya Teknolojia kusonga mbele, kwani kama taifa tusipojipanga kimkakati, Tanzania itaachwa nyuma.

‘E-Learning Africa’ linafanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ukishirikisha nchi 65 za Afrika na nje ya Afrika, wakiwemo Mawaziri wa Elimu takribani 20, ukijikita katika masuala ya kutumia teknolojia kukuza sekta ya elimu na kutanua wigo wa njia za ufundishaji barani Afrika.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa Kongamano hilo, Prof. Mkenda amebainisha kuwa, Serikali kupitia Wizara yake ina mipango chanya na endelevu juu ya ‘E-Learning Africa’, ambayo wataitangaza Jumatatu wakati wa kuwasilishwa kwa Bajeti ya Wizara yake na kwamba baada ya miaka mitano, taifa litakuwa miongoni mwa nchi za mfano barani Afrika.

“Lengo la mkutano huu ni kubadilisha mawazo, kuelezana uzoefu wa namna ya kulipeleka mbele bara la Afrika na nchi zetu katika teknolojia hii ambayo inakua kwa kasi sana. Mabadiliko ya teknolojia ni makubwa na yanaenda kwa kasi ya ajabu sana, yapo mambo hata katika mfumo wa elimu itabidi yaangaliwe upya, mengine yabadilishwe.

“Kwa jinsi Teknolojia inavyoendelea, nasi kama taifa tuitumie kusonga mbele, ukweli ni kuwa, dunia inavyoenda, Tanzania tusipojipanga kimkakati, tutaachwa nyuma. Tumeona nchi 10 Bora Afrika katika teknolojia, Tanzania haimo, lakini bahati nzuri pia kuwa katika nchi 10 za mwisho, Tanzania pia hatumo.

“Hii maana yake ni kuwa Tanzania tupo pazuri kiasi. Tayari tuna mkakati, tuna muongozo na hatua nyingine tutazitangaza kwenye bajeti yetu inayosomwa Jumatatu bungeni jijini Dodoma, ambayo tuna uhakika baada ya miaka miwili, mitatu hadi mitano, Tanzania tutakuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vema katika elimu kwa njia ya kidigitali,” alisema.

Akizungumzia kongamano hilo, Prof. Mkenda alisema washiriki wanajifunza E-Learning Africa yaani jinsi ya kutumia taaluma ya kidigitali kwenye ufundisjaji na jinsi ya kufundisha taaluma kidigitali katika shule na vyuo vya Afrika, mkutano ambao umekuwa ukifanyika kila mwaka na kwamba hii ni mara ya pili kwa Tanzania kuwa mwenyeji.

“Mkutano unaenda vizuri sana, kumekuwa na mwitikio mkubwa ambao hata sisi wenyeji umetushangaza, tumepata mawaziri 20 waliokuja kushiriki hapa na tunaishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki namna ilivyowapokea vema washiriki na nimeongea na waziri mmoja mmoja na wenyewe wamefurahishwa na namna mapokezi yao yalivyo.

“Kwa sababu ya maendeleo ya teknolojia, kwa mfano sasa hivi tunavyofundisha darasani ukiwa na wanafunzi 45 au 60, unawafundisha wote kwa pamoja ukichukulia kuwa wote wako sawa, lakini katika teknolojia hii, inatoa fursa ya kufundisha kila mwanafunzi kwa kasi yake, anayeenda taratibu na anayejifunza kwa haraka haraka.

“Kupitia aina hiyo ya ufundishaji, mkufunzi unakuwa na uwezo wa kufundisha kwa namna nyingi, kwa mfano unaweza kuwa na Mwalimu anafundisha Benjamin Mkapa hapa, siku hiyo akaunganishwa na darasa lingine lililopo Tandahimba kwa mfano, ili afunsdishe somo lingine kule wakamsikiliza na kumuona,” alibainisha Prof. Mkenda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *