‘Kariakoo Derby’ sasa kupigwa Juni 15, Yanga SC yasisitiza kutocheza

WAKATI Uongozi wa Yanga ukisisitiza kutocheza mechi namba 184 dhidi ya Watani wao wa Jadi Simba SC, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), limetangaza tarehe mpya ya mchezo huo ulioahirishwa Machi 8 na Sasa utapigwa Juni 15 saa 11 jioni kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Yanga walikuwa wenyeji wa mchezo wa Machi 8, ambao hata hivyo uliahirishwa na Mamlaka za Soka nchini, baada ya Simba kutishia kutoingiza timu kwa madai ya kupinga ukiukwaji wa kanuni inayomtaka mgeni kufanya mazoezi kwenye uwanja husika siku moja kabla mchezo. Simba walilalamika kuzuiwa na Yanga kutojifua usiku wa Machi 7.

Yanga walipinga uamuzi huo na kutuma malalamiko yao kwa Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS), ambayo katika uamuzi wake, iliitaka Yanga kukata rufaa kwa Mamlaka za Soka nchini, kabla ya kwenda CAS, lakini wakasisitiza hawatokata rufaa TFF kwa kuwa hawana imani nayo, lakini ikasisitiza hawatocheza na Simba tena msimu huu.

Mapema leo Mei 6, TPLB imetoa ratiba ya mechi zilizosalia kwenye Ligi Kuu ya NBC pamoja na CRDB Bank Federation Cup, ambapo mchezo kati ya Yanga dhidi ya Simba, sasa kupigwa Juni 15, 2025, saa 11 jioni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba ya TPLB, Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara inatarajiwa kumalizika Juni 22, 2025, huku fainali ya CRDB Bank Federation Cup ikopigwa kati ya Juni 26 na 28.

Bingwa wa Ligi Kuu huiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2025/26), huku bingwa wa CRDB Federation Cup akiiwakilisha katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC 2025/26).

Iwapo itang’ang’ania na kutekeleza msimamo wa kutocheza mechi dhidi ya Simba, Yanga ambayo Iko hatua ya nusu fainali ya CRDB Bank Federation Cup, itakuwa hatarini kupoteza alama tatu na ubingwa wanaoushikilia kwa misimu mitatu mfululizo.

Aidha, Yanga inaweza kukupambana na adhabu mbalimbali ikiwemo kupokwa pointi 15 ama kushushwa daraja, ambazo katika msisitizo wao walioutia Mei 5, Wananchi wamesisitiza kuwa wako tayari kuzikabili, kuliko kucheza mechi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *