Singida Black Stars kuivaa Simba CRDB Federation Cup, JKT Tanzania yaisubiri Yanga

HATIMAYE mpinzani wa Simba katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania ‘CRDB Bank Federation Cup, amejulikana ni Singida Black Stars, baada ya ‘Walima Alizeti,’ hao kushinda robo fainali yao jioni ya leo kwa mabao 2-0 walipowaalika Kagera Sugar ya Kagera kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida.

Nao Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa JKT Tanzania wametangulia hatua hiyo leo baada ya kuichapa Pamba Jiji ya Mwanza bao 3-1 kwenye dimba la Meja Jenerali Isamuhyo, Dar na Sasa wanasubiri mshindi wa robo fainali ya Jumanne hii kati ya Yanga na Stand United ya Shinyanga.

Mjini Singida, wenyeji Singida Black Stars walikuwa nyumbani kuwaalika Kagera Sugar, ambako dakika 90 zimekamilika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, yaliyofungwa na Victorien Adebayor na Jonathan Sowah, matokeo yanayoikutanisha Singida Black Stars dhidi ya Simba SC katika nusu fainali.

Maafande wa JKT Tanzania wakiwa Meja Isamuhyo wameibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Pamba Jiji ya Mwanza, shukrani kwa mabao ya Yunus Lema (aliyejifunga) na Mohammed Bakari aliyetikisa nyavu mara mbili, huku bao la kufutia machozi la Pamba, likiwekwa kambani na Henry Msabila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *