SHUKRANI zote kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya kufanikiwa kutimiza kile alichokisema cha kukamilisha Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere(Julius Nyerere Hydro Power Project-JNHPP).
Kukamilika kwa mradi huu kulikotimizwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kunaifanya nchi iwe na umeme wa uhakika na hapa ndipo kauli ya ‘Kazi Iendelee’ inatimizwa kwa vitendo.
Jana akiwa Bungeni, Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikaririwa akisema; “Ujenzi wa mradi huu wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 kwa siku umekamilika. Hadi Machi 2025 jumla ya megawati 2,115 zimeunganishwa kwenye gridi ya taifa na hivyo kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya taifa kufikia megawati 4,031.7.
“Kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika mradi huo kumeongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwa chachu ya kasi ya maendeleo ya nchi.
“Katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Februari 2025, Serikali pia imeunganisha umeme katika vijiji 4,071 kwa gharama ya Shilingi bilioni 1,593 na hivyo kuwezesha vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara kuunganishwa na umeme.
“Hatua inayofuata baada ya kukamilisha mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote, ni kupeleka umeme kwenye vitongoji ambapo jumla ya vitongoji 33,657 kati ya 64,359, sawa na asilimia 52.3 vimeunganishwa na huduma ya umeme.
“Usambazaji wa umeme katika vijiji na vitongoji utawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zinazohitaji nishati ya umeme zikiwemo kuchomelea vyuma, useremala, kuchakata nafaka na kuchenjua madini.”
Ndivyo ambavyo anavyokiri Mhandisi Manala T. Mbumba ambaye amebobea katika suala la nishati safi, huku akiwa na mkono wake katika ujenzi wa Bwawa la Nyerere.
Habari za kukamilika kwa mradi huo zilianza kutolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko, aliyetamka wazi mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa umekamilika.
Alitamka wazi kuwa, mitambo yote tisa inafanya kazi na kukamilika kwa mradi huo kumechangiwa na maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliupokea mradi ukiwa katika asilimia 33 ya utekelezaji wake na ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake ameweza kuukamilisha.
Kulikuwa na upinzani mkubwa wakati wa kuanzisha mradi huu, lakini kutokana na ujasiri wa Serikali kusimamia maslahi ya Watanzania ikafanikiwa kuuanzisha na sasa unakuja kuleta matunda bora kwa wote.
Likiwa moja ya mabwawa makubwa ya kufua umeme barani Afrika, Bwawa la Umeme wa Maji la Julius Nyerere ni kichocheo tosha cha maendeleo nchini.
Anachosema Mhandisi Manala
Mhandisi Manala Tabu Mbumba ambaye anajua mengi juu ya bwawa hilo na ni hazina ya Taifa katika mambo ya nishati alisema, Afrika imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za nishati jadidifu, kama vile jua, upepo, na maji, lakini uwekezaji katika sekta hii bado ni mdogo, hali inayohitaji juhudi za kushirikiana kikanda na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje katika teknolojia za nishati safi.
Mhandisi Manala aligusia changamoto kubwa ya upatikanaji wa nishati vijijini, akisema kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu barani Afrika hawana umeme na sehemu kubwa ya watu hao ni kutoka vijijini, lakini kukamilika kwa Bwawa la Nyerere kunaenda kuiweka Tanzania katika ramani nyingine.
“Hapa lazima umpe shukrani za dhati Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwani amefanya kile ambacho kila mtu anayeitakia mema nchi hii anakipenda. Hapa lazima tumshukuru, hili ni jambo kubwa na kulisema hadharani,” alisema Mhandisi Manala.
Alisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia ya mini-grids na off-grid inayotumia vyanzo vya nishati jadidifu ili kuwafikia wananchi wa vijijini kwa bei nafuu.
Pia, alizungumzia umuhimu wa ushirikiano wa kikanda katika miradi ya nishati, akisisitiza kwamba miradi kama mabomba ya gesi, usambazaji wa umeme wa kikanda, na sera zinazowezesha biashara ya nishati baina ya nchi zitasaidia kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa nishati.
Kwa upande mwingine, Mhandisi Manala alisisitiza haja ya kuwekeza katika teknolojia za kisasa na kukuza wataalamu wa ndani katika sekta ya nishati.
Alisema serikali, sekta binafsi, na taasisi za elimu zinapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa tuna nguvu kazi inayoweza kutumia, kutengeneza na kudumisha teknolojia mpya za nishati.
Katika kujibu changamoto za mabadiliko ya tabianchi, alieleza kuwa sekta ya nishati ina mchango mkubwa katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na kulinda mazingira.
Aliongeza kuwa Afrika, ikiwa ni mojawapo ya mabara yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi, inapaswa kuwa kinara wa kuonyesha mfano wa kupunguza utegemezi wa mafuta na kuhamia kwenye nishati safi.
Mhandisi Manala pia alisisitiza kwamba ili kufanikisha ajenda ya nishati safi, ni muhimu kuvutia wawekezaji kwa kutoa motisha kama punguzo la kodi na usaidizi wa kifedha kwa miradi ya nishati safi.
Pamoja na mambo mengine mtaalamu huyo alisema, Tanzania iwe na fursa za kuonyesha hatua inazochukua katika kuimarisha sekta ya nishati, ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ya umeme wa maji na juhudi za kukuza nishati jadidifu.
“Namshukuru Mungu kwa kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kututeulia kiongozi mchapa kazi.Dk.Doto Biteko Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na kumwekaeneo kama hili muhimu naamini analimudu na kuhakikisha Watanzania tunatimiza ndoto zetu. Bila nishati endelevu, maendeleo endelevu ni ndoto,” alisema Mhandisi Manala.
Hiki ndicho
Kituo cha Umeme wa Maji cha Julius Nyerere (Julius Nyerere Hydro Power Project-JNHPP) ni mradi mkubwa wa umeme wa maji uliojengwa kwenye Mto Rufiji.
Mradi huo una uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 za umeme, na kuongeza uzalishaji wa umeme nchini. Mradi huu unalenga kupunguza utegemezi wa umeme kutoka vyanzo vya nje, kuboresha huduma za umeme kwa wananchi na viwanda, na kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi.
Kukamilika kwa mradi huu mkubwa kunapelekea kuwa na umeme wa gharama nafuu, uhakika na vilevile kuchangia katika pato la Taifa. Mradi wa Julius Nyerere – JNHPP umeajiri wafanyakazi zaidi ya 11060, asilimia 90 ikiwa ni Watanzania na asilimia 10 wakiwa ni wageni.
Mkombozi kwa wote
Upatikanaji wa umeme wa Julius Nyerere ni sawa na ongezeko la asilimia 136 zaidi ya uwezo wa sasa wa megwati 1,694.55 kwenye gridi ya Taifa. Mradi huu wa Bwawa la Julius Nyerere ni mkubwa Afrika Mashariki na wa 4 kwa ukubwa barani Afrika.
Ulivyogawanywa
Mradi huu umejengwa katika maeneo manane hadi uanze kuzalisha umeme kama ifuatavyo:- 1. Kazi za kuchepusha mto (Diversion works), 2. Tuta Kuu (Main Dam), 3. Njia za maji ya kuendesha mitambo (Power Waterways), 4. Jengo na mitambo (Powerhouse), 5. Kituo cha kusafirisha umeme (Switchyard), 6. Matuta madogo (Saddle Dams), 7. Makazi ya kudumu (Operation Village) na 8. Barabara na daraja la kudumu (Permanent Roads & Bridge).
Bwawa hili lina mahandaki matatu yenye urefu wa mita 12 kwa 17 na njia tatu za kupitisha maji, ambayo mbele yanagawanyika na kuwa na mitambo tisa ya kuzalisha umeme. Kila mtambo utazalisha megawati 235, ambapo mitambo 9 kwa ujumla itazalisha megawati 2,115.
Kwa upande wa tuta la Bwawa la Nyerere kwenye kitako chini ukuta una upana wa mita 100 na ukuta huo unakwenda unapungua hadi juu ambako una upana wa mita 10. Ukuta wa tuta una urefu wa mita 190 kutoka usawa wa bahari. Juu ya ukuta huu wa bwawa hili itakuwapo barabara inayopitisha magari.
Mito inayojaza maji
Mito kutoka mikoa 11 inajaza maji katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mito mikubwa mitatu inayojaza maji kwenye Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere inaanzia katika mikoa 10. Mito hiyo ambayo ni Ruaha, Kilombero na Luwengu, inakusanya vijito kutoka mikoa ya Tabora, Singida, Dodoma, Iringa, Mbeya, Morogoro, Pwani, Ruvuma, Dar es Salaam na Njombe. Mito kutoka mikoa hii yote inamwaga maji katika Bonde la Mto Ruvu.
Bwawa hili linalokadiriwa kudumu kwa miaka 100 na zaidi, limeleta faida kubwa nchini. Saruji yote iliyojenga Bwawa la Nyerere ambayo ni tani 850,000, nondo tani 70,000 na udongo maalumu tani 250,000, ajira 12,298 vyote hivi vimekuwa vya manufaa kwa Tanzania.
Ujazo wa bwawa
Bwawa hili lenye urefu wa kilomita 100 kutoka ncha moja kwenda nyingine na ukubwa sawa na nusu ya Mkoa wa Dar es Salaam, litajaza maji wastani wa lita za ujazo bilioni 33.2.
Uwekezaji huu mkubwa wa Sh trilioni 6.5 katika Bwawa la Nyerere unatokana na ukweli kwamba umeme wa maji ndio umeme rahisi kuliko umeme wowote hapa duniani.
Gharama kupungua
Gharama ya kuzalisha uniti moja ya umeme wa maji ni Sh 36 na baada ya muda mrefu gharama hizi hushuka, ilhali kwa sasa kupitia vyanzo mbalimbali Tanzania inazalisha uniti moja kwa wastani wa senti 10.7 za dola sawa na Sh 249 kwa uniti.
Misri inazalisha umeme kwa senti 4.6 za dola sawa na Sh 107, Afrika Kusini senti za dola 7.4 sawa na Sh 172, Ethiopia wanatumia maji senti za dola 2.4 sawa Sh 56 na India senti za dola 6.8 sawa na Sh 158.
Ukiacha udhibiti wa mafuriko na kuongezeka kwa umeme kwenye gridi ya taifa, ongezeko hili la umeme linaongeza mapato ya TANESCO na Serikali.
Kuingia kwa megawati 2,115 ina maana mapato ya mauzo ya umeme ya TANESCO yanaongezeka mara mbili, hivyo kuongeza mapato ya shirika na serikali. Mradi huu pia utaongezea ufanisi kilimo cha umwagiliaji kwa wastani wa hekta 450,000. Mradi utaleta ulinzi bora wa mazingira.
Pongezi kwa Rais Samia
Mhandisi Manala Tabu Mbumba anasema, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anaingia madarakani, alikuta mradi huu umeanza na ukiwa umefanywa kwa asilimia 33 ya utekelezaji wake, lakini ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi ameweza kuukamilisha.
Alisema, hii inathibitisha nia ya dhati ya Rais Dkt. Samia katika kutekeleza kwa vitendo ahadi na maono yake, huku mwenyewe akijipambanua vyema kuwa ni mtetezi na mpambanaji wa nishati safi na salama.
Takwimu za nishati kwa Afrika zinaonesha kuwa hadi mwaka 2022 asilimia 83 ya watu milioni 685 walikuwa
hawajafikiwa na nishati hiyo.
Mradi wa Bwawa la Kufua umeme la Julius Nyerere ulianza Disemba 15 2018 baada ya kusainiwa mkataba. Kazi rasmi za
ujenzi zilianza 14 Juni 2019 hadi kufikia hatua ya kukamilika hivi sasa.
