NA MWANDISHI WETU, DAR
FAMILIA ya Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, imefuturisha Wateja wa benki hiyo, Waumini wa Dini wa Kiislamu, Viongozi wa Dini na Serikali, ikiwa ni muendelezo wa utamaduni chanya familia hiyo na taasisi hiyo kujumuika pamoja wakati wa Mfungo wa Ramadhani.

Hafla hiyo imefanyika Jumatano Machi 12, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa dini wakiongozwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir bin Ally Mbwana, huku upande wa viongozi wa Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Akizungumza wakati wa Iftar hiyo, Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir alimpongeza Nsekela na taasisi yake kwa kudumisha utamaduni wa kufuturisha Waumini katika kipindi cha Ramadhani, ambayo ni Nguzo ya Nne kati ya Tano za Kiislamu, na kwamba kitendo hicho kina malipo makubwa sio tu kwa mfungaji, bali hata mfuturishaji.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, huku akinukuu Hadithi ya Mtume Muhammad, kutoka kwa Tirmidhiy, Ibn Majah, Sheikh na Mufti Mkuu wa Tanzania, alisema: “Mwenye kumfuturisha aliyefunga atapata ujira na malipo makubwa sawa na yule aliyefunga, bila hata ya kupungua chochote katika ujira na malipo ya aliyefunga.”
“Nimshukuru sana na nimpongeze Bwana Nsekela kwa jambo hili kubwa alilolifanya yeye na familia yake na taasisi yake, kwani hili ndilo alilohimiza Mtume. Kwahiyo malipo makubwa unayoyapata, moja wapo ni kubarikiwa na Mwenyezi Mungu na tunamuomba akujaalie uendelee na moyo huu,” alisema Mufti Mkuu.
Kwa upande wake, Nsekela alimshukuru Mufti Mkuu na waalikwa wengine kwa kuhudhuria hafla hiyo, huku akiwaombea Waumini wa Kiislamu na waalikwa wote kuwa na mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ambao kwa sasa upo katika 10 la pili la ‘maghufirrah.’

“Huu ni mwezi ambao Waumini wa Kiislamu duniani kote wanafunga kutekeleza moja ya nguzo za Dini yao, lakini pia ni mwezi ambao unatukumbusha kuwa na upendo katika kumcha Mwenyezi Mungu na Iftar hii ya leo ni sehemu ya shukrani za familia yangu kwa Mungu,” alisema Nsekela na kuwashukuru waliohudhuria.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema amefarijika sana kwa aina ya hafla iliyofanywa na CEO Nsekela, ambaye alimuombea kheir ashiriki Ibada ya Hijja mwaka huu wa 2025, ili mwakani atakapofanya hafla hiyo tena, hadhi yake iwe ya Al Hajji Abdulmajid Nsekela.
