Na Mwandishi Wetu, Tanga
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB), imegawa bure miche ya Mkonge milioni 12 kwa wakulima katika kipindi cha miaka minne katika maeneo mbalimbali inayolima Mkonge nchini.
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC), katika eneo la kitalu cha kuzalisha miche ya Mkonge TARI Mlingano mkoani Tanga, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Saddy Kambona amesema hatua hiyo ni msukumo wa Serikali ya Awamu ya sita ambapo Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua mbegu za Mkonge zigawiwe bure kwa wakulima wadogo na kuuzwa kwa bei ya ruzuku.

Amesema wakati wanaanza kampeni ya kuhamasisha wakulima wadogo mwaka 2022, Serikali ya Awamu ya Sita ilianza kutoa mbegu za ruzuku kwa kuongezea zile zilizoko kwenye kitalu zilikuwa takribani hekta 600 zinazozalisha miche zaidi ya milioni mbili na nusu kila mwaka.
“Baada ya kampeni hiyo iliyoasisiswa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, uhitaji ukawa mkubwa na hata alipoingia madarakani Mhe. Dkt. Samia ile nguvu na msukumo kama alivyosema mwenyewe kazi iendelee hakuna ambacho kilikuwepo akakiacha bila kukiendeleza.
“Kwa hiyo akafanya mwendelezo kusukuma hili zao liende mbele zaidi kwenye uzalishaji wa mbegu za vikonyo kwa maana ya kwenye vitalu, akaanza ujenzi wa maabara ya kisasa ya kuzalisha miche ya Mkonge (tissue culture) ambayo itakuwa na uwezo wa kuzalisha miche milioni 10 kwa mwaka.
“Lakini pia alitoa fedha Sh milioni 500 kwa ajili ya kutafuta mbegu bora nyingine za matoto ili kuwafikishia wakulima bure.
“Lengo lilikuwa ni kupata sehemu kubwa ya mbegu na kwa sasa miche hiyo pia inauzwa kwa bei ya serikali au bei ya ruzuku kwa maana kwamba gharama halisi ya uzalishaji inafika Sh 225 kwa mche lakini kwa ruzuku ambayo Mhe. Rais ameitoa mwananchi ananunua kwa bei ya Sh 130,” amesema Mkurugenzi Kambona.
