TMA: Kimbunga ‘Jude’ kuleta mvua kubwa

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “Jude” katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Machi 10, 2025 inaeleza kuwa uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa kimbunga hicho kitaingia nchi kavu katika eneo la Msumbiji mchana wa leo Machi 10, 2025 na kupungua nguvu yake.

Hata hivyo, kimbunga Jude kinatarajiwa kurejea tena baharini na kuimarisha nguvu yake katika kipindi cha kati ya tarehe 13 hadi 15 Machi 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kutokana na mwelekeo na umbali wake kimbunga Jude hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja hapa nchini.

Hata hivyo, uwepo wa kimbunga hicho katika eneo la rasi ya Msumbiji unatarajiwa kuchagiza mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kusababisha ongezeko la mvua katika maeneo mbalimbali.

Vilevile, uwepo wa kimbunga hicho unaenda sambamba na kuanza kwa msimu wa mvua za masika, 2025 katika maeneo yapatayo misimu miwili ya mvua kwa mwaka kama ilivyotabiriwa awali na taarifa kutolewa kwa hiyo Umma mnamo Januari, 2025.

Mamlaka inawashauri watumiaji wa bahari na jamii kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa zake utabiri kutoka TMA na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga Jude na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *