Tanzania na Marekani zasuka mkakati kukuza maendeleo ya kiuchumi

Tanzania na Marekani zajadili mkakati wa kukuza uchumi katika Kongamano la maendeleo ya kiuchumi kuchochea mwingiliano wa biashara na uwekezaji lililozikutanisha takribani kampuni 40 kutoka nchi hizo mbili jijini Dar es Salaam Machi 11, 2025.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amehudhuria kongamano hilo kama mgeni maalum na kuzungumza na wafanyabiashara na wawekezaji hao wanaojumuisha kampuni 19 za Kimarekani na 20 za Kitanzania zenye kuangalia fursa mbalimbali katika sekta za teknolojia, kilimo, viwanda, ujenzi/nyumba na elimu.

Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Kombo amezisisiza kampuni za Marekani kutumia fursa hii pekee kuongeza ushirikiano katika teknolojia za kilimo kwani Tanzania ina ardhi yenye rutuba kwa mazao aina nyingi. Pia kutambua kuwa huu ndio mwanzo wa uhusiano wa muda mrefu na Tanzania na hivyo ni vyema kuwa na mwanzo ulio bora.

Mheshimiwa Kombo ameeleza kuwa mkoa wa Dodoma una uhitaji mkubwa sana wa nyumba za makazi zaidi ya 120,000 na hivyo kwa wale wanaotazamia kuwekeza katika ujenzi wa nyumba, wauone mkoa huu kama moja ya maeneo yenye tija kwa aina hiyo ya uwekezaji na biashara.

Katika sekta ya Elimu Waziri Kombo ameeleza gharama zinazotumika kuwasafirisha wanafunzi kufuata masoma katika vyuo vya Kimarekani na kueleza kuwa endapo matawi ya baadhi ya vyuo vikuu vya Marekani yatafunguliwa nchini, basi itasaidia kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili, na kupunguza gharama kubwa za kusafiri kwenda nje.

Jitihada hizi zinazosaidia kuinua maisha ya Mtanzania mmoja mmoja zinatajwa kuwa chachu ya maendeleo chanya na hivyo kupunguza wimbi la rushwa.

Aidha, Waziri Kombo amesema katika kuimarisha ushirikiano huu wa kukuza maendeleo ya kiuchumi, ipo haja ya kupitia tena mfumo wa utoaji wa visa ya Marekani kwa Watanzania ili uwe rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania.

Kongamano hilo limeandaliwa na Ubalozi wa Tanzania Marekani chini ya uongozi wa Balozi Elsie Kanza kwa kushirikiana na taasisi ya Taifa ya Maendeleo ya kiuchumi ‘National Institute Economic Development (NIMED)’, taasisi ya Kimataifa ya Miji Dada ‘Sister Cities International’ – (SCI) ya nchini Marekani na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *