NA MWANDISHI WETU
MNYUKANO Mkali umeibuka nje ya uwanja, pande mbili zikivutana na kutia shaka uwepo wa pambano la Wapinzani wa Jadi wa soka la Tanzania, Yanga na Simba, linalotarajiwa kufanyika kuanzia saa 1:15 usiku wa leo Machi 8, kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Tishio la kutowepo pambano hilo limeanzia jana usiku, baada ya Wekundu wa Msimbazi Simba kuiandikia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), iliyo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwamba hawatoshiriki mchezo huo, kutokana na kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho jana usiku kwenye dimba hilo kama kanuni ya 17(45) inavyowaruhusu.
Katika barua yao kwa mamlaka hizo za soka, Simba ambayo ilifika uwanjani hapo na mabasi mabwili (la klabu na la Kampuni ya BM), imesema ilifika Uwanja wa Benjamini Mkapa saa 1 usiku, lakini Meneja wa Uwanja huo akawazuia kuingia kufanya mazoezi kwa alichodai hana maelekezo ya Kamishna wa Mchezo.
“Pamoja na Kamishna wa mchezo kufika baadaye, lakini mabaunsa wa klabu ya Yanga walivamia msafara wa Simba SC na kufanya vurugu ikiwemo kuuzuia kuingia uwanjani. Jitihada za uongozi wa Simba kupata ufumbuzi wa suala hilo hazikuzaa matunda kwa zaidi ya masaa mawili na hivyo kuamua kuondoka kwa sababu za kiusalama.
“Kufuatia ukiukwaji huo wa Taratibu za Mchezo, Simba haitoshiriki mchezo husika na haki zote zimehifadhiwa. Simba inahimiza kuchukuliwa kwa hatua stahiki dhidi ya wahusika wote wa sakata hili,” imemaliza taarifa ya Menejimenti ya Simba juu ya mtafaruku huo, kwenda kwa umma na mamlaka za soka nchini.
Mapema leo, TFF kupitia Bodi ya Ligi imejibu barua hiyo ya usiku wa manane, ambako imekiri kwamba ni haki kwa timu ngeni yoyote kutumia uwanja wa mechi kwa mazoezi wakati sawa na wa mechi husika siku moja kabla, lakini ikaonya kuwa Simba inapaswa kushiriki mchezo huo bila kukosa na kuachia mamlaka hizo kuamua kupitia kanuni.
“TFF imepokea barua ya malalamiko kutoka Simba SC kuhusu changamoto zilizojitokeza kuelekea mechi dhidi ya Yanga. Pamoja na hayo, tunapenda kuwajulisjha kwamba kwa mujibu wa Kanuni ya 15(10) ya Ligi Kuu, timu yoyote ina wajibu wa kushiriki michezo yote inayoratibiwa na TFF bila kukosa, isipokuwa kukiwepo sababu maalum zilizoidhinishwa na TFF.
“Aidha, kutoshiriki mchezo husika kunaweza kusababisha adhabu kulingana na Kanuni ya 16(1), inayohusu maamuzi dhidi ya timu isiyotii ratiba ya ligi. Pia kwa mujibu wa Kanuni ya 17(45), inayotaka haki ya kufanya mazoezi uwanjani, tutahakikisha masuala hayo yanafuatiliwa kwa kina na hatua za kinidhamu zinachukuliwa dhidi ya waliohusika kuivunja.
“Hivyo basi, kwa kufuata Kanuni za Shirikisho, tunawaagiza (Simba) kuendelea na taratibu za mchezo kama ulivyopangwa ili kuheshimu ratiba ya Ligi Kuu ya NBC na kuzingatia maslahi ya mashabiki, wadhamini na ligi kwa ujumla. Malalamiko kuhusu changamoto zilizojitokeza yatafanyiwa kazi kwa wakati unaofaa,” imesisitiza TPLB.
Je, Kitapigwa au Kitasusiwa? Ni suala la kusubiri na kuona, muda utatoa majibu.
