KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao
chake cha leo Machi 8, 2025 imepitia shauri la klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye uwanja
wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa
Ligi Kuu ya NBC (Young Africans SC vs Simba SC) uliopangwa kufanyika kwenye uwanja huo leo
kuanzia saa 1:15 usiku.

“Katika shauri hilo, klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajwa
hapo juu, huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwasababu imezuiliwa kutumia
haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu
za Mchezo.
Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo (ambao
walishuhudia tukio hilo), kutuma taarifa ya tukio haraka ili hatua zinazostahili ziweze
kuchukuliwa, ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharura cha Kamati ya Uendeshaji na
Usimamizi wa Ligi.
Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwemo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine,
Kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba, wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye
Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu, haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo, timu mwenyeji wala
mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika uwanja huo ili maandalizi ya
kikanuni yafanyike.
Katika taarifa hizo, Kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura
kuwa ni wa klabu ya Yanga, walishiriki tukio la kuzuia basi la klabu ya Simba kuingia uwanjani
kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Kwasababu pia Bodi ilipokea taarifa ya Ofisa Usalama wa mchezo ambayo imeainisha matukio
kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi, na
kwamba baadhi ya matukio yanahitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati, Bodi
ya Ligi kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo
tajwa hapo juu kwa mujibu wa Kanuni ya 34:1(1.3) ya Ligi Kuu kuhusu Kuahirisha Mchezo, ili
kutoa nafasi ya kupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki.
Bodi itatoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo na kutangaza tarehe ya mchezo huo mapema iwezekanavyo.
Imeeleza taarifa ya Bodi ya mchana huu.
