Maofisa Ugani kupewa mafunzo ya kilimo ikolojia

Ofisa Ugani Kija Somanda akizungumza na washiriki wa mafunzo ya wakulima na wafugaji wanaofanya kilimo ikolojia chini ya mwamvuli wa Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) kwa kushirikiana na Bio Vision kutoka Kenya kupitia mradi wa Mkulima Mbunifu.

Erica Rugabandana Mhariri Mkuu wa Jarida la Mkulima Mbunifu akizungumzia shughuli zilizofanywa mwaka 2024.

Mkurugenzi wa SAT, Janet Maro akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.

Washiriki wa mafunzo ya ufugaji na ukulima wa kuzingatia ikolojia.

Na Irene Mark, Dodoma

KATIKA kukiendeleza kilimo ikolojia, Serikali imedhamiria kuwapa mafunzo maofisa ugani wake 6,748 nchi nzima ili kuwafundisha wakulima kwenye vijiji vyao.

Hayo yamesemwa leo Machi 4, 2025 na Ofisa Huduma za Ugani, Idara ya Maendeleo ya mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Kija Somanda wakati wa mafunzo ya wakulima na wafugaji wanaofanya kilimo ikolojia chini ya mwamvuli wa Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) kwa kushirikiana na Bio Vision kutoka Kenya kupitia mradi wa Mkulima Mbunifu.

Warsha ya Kilimo ikolojia na Jarida la Mkulima Mbunifu yanayoendelea jijini Dodoma, yamewakutanisha wakulima nanwafugaji viongozi wanaofanya kilimo ikolojia cha mazao tofauti kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.

Somanda amesema mradi wa mafunzo kwa maofisa ugani ni sehemu ya majukumu ya Wizara ya Kilimo huku alisisitiza mradi wa mwaka huu utahusisha kilimo ikolojia zaidi kwa maofisa ugani.

“Mradi huu wa kilimo ikolojia tunaufanya nchi nzima. Maofisa ugani watafindishwa namna sahihi ya kutunza udogo na rutuba yake kwa njia za asili.

“…Kwa mujibu wa muongozo wa mradi huu maofisa ugani watafundishwa pia jinsi ya kutunza mbegu za asili, kutengeneza mbolea na viwatilifu kwa kutumia vitu vya asili,” amesema Somanda.

Ofisa ugani huyo ameweka bayana kwamba serikali imeandaa soko la mazao na mifugo iliyotunzwa kwa njia za asili huku akisisitiza kuwepo kwa soko kubwa la ndani na nje ya nchi.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa SAT, Janet Maro amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuibua mada bunifu za kuboresha kilimo ikolojia kwenye maeneo yao kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa.

Mkurugenzi huyo amesema washiriki wa mafunzo hayo wanafundishwa miongozo na kanuni za kilimo ikolojia kama inavyotakiwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO).

“Nawapongeza sana kwenye mafunzo ya mwaka jana 2024 mlitoka na mada bunifu na nzuri ambazo zilitumika kuandika makala bora zilizomsaidia mkulima na mfigaji kufanya shughuli zake kwa njia za asili na na kutunza mazingira,” amesema Maro.

Baadhi ya wakulima na wafugaji wanaopata mafunzo hayo wamewashukuru SAT na Bio Vision kwa kuwatembelea, kuwafundisha nadharia na vitendo namna bora ya kufanya ufugaji na kilimo ikolojia huku wakitunza mazingira na kuinua uchumi wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *