CRDB Foundation yazindua Mradi wa Uunganishwaji Wajasiriamali Tanzania na Fursa za AfCFTA

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), wamezindua rasmi Mradi wa Uunganishwaji wa Wajasiriamali Wadogo wa Tanzania na Fursa za Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), ikiwa ni mwaka mmoja tangu taasisi hizo mbili ziliposaini mkataba wa ushirikiano katika kipindi cha miaka mitano.

Januari 17, 2024, CRDB Foundation na UNDP, walisaini makubaliano hayo yakigusa maeneo matano ya Uwezeshaji Vijana na Wanawake/Biashara Changa, Ufadhili wa Miradi Endelevu, Utekelezaji wa Programu za Pamoja za Kutafuta Rasilimali za Utekelezaji wa Miradi na Kushirikiana kwa Utaalam Maalum na Msaada wa Kiufundi

Baada ya mkataba huo, leo Machi 2, CRDB Foundation na UNDP wamezindua Mradi wa Uunganishwaji Wajasiriamali wa Kitanzania na AfCFTA, ukiwa na malengo manne, ambayo yamepongezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, aliyemwakilisha Waziri Suleiman Jafo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Waziri Kigahe aliishukuru Menejimenti ya Benki ya CRDB kupitia Taasisi ya CRDB Foundation, kwa kushirikiana na UNDP na kubainisha kuwa Mkataba wa AfCFTA ni kati ya Miradi ya Kimkakati ya Umoja wa Afrika, unaolenga kulifanya Bara la Afrika kuwa soko moja la bidhaa na huduma.

“Ni mradi utakaochangia katika kasi ya mchangamano, ushirikiano na muingiliano wa kibiashara baina ya nchi wanachama, na hivyo kunufaika na soko lenye watu zaidi ya bilioni 1.5 na kutokana na manufaa ya mkataba huu, Bunge letu liliridhia mnamo Septemba 2021 na Tanzania kuwa nchi iliyokidhi vigezo vya kushiriki katika Soko Huru la Afrika.

“Uamuzi huu ulichukuliwa na Serikali lengo likiwa ni moja tu, kuhakikisha tunafungua fursa kwa wajasiriamali wetu nje ya mipaka kunufaika na masoko na ili kunufaika na mkataba huu, kwa ukubwa unaostahili, lazima watu wawe na elimu sahihi, maarifa ya kutosha kuvuka mipaka kuzifuata fursa hizo mahali ziliko katika nchi 55 za Afrika

“Kinachofanywa na CRDB leo ni miongoni mwa mikakati ya kuwawezesha wajasiriamali wetu kumudu soko la ushindani dhidi ya wenzao kutoka mataifa mbalimbali Afrika, kwa mara nyingine niwapongeze sana CRDB kupitia CRDB Foundation kwa kushirikiana na UNDP kuwanyanyua wajasiriamali nchini.

“Serikali inaipongeza CRDB Foundation kwa kuja na Mradi wa Kuwawezesha Wajasiriamali wetu Wanawake na Vijana kunufaika na AfCFTA, kwani tunaamini kuwa makundi hayo mawili yanaunda zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wote, hivyo ni muhimu sana, kwani ndio makundi tunayoyategemea katika uchumi wetu,” alisisitiza Naibu Waziri Kigahe.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa, alianza kwa kumshukuru Naibu Waziri Kigahe kushiriki uzinduzi huo na kusema uwepo wake katika hafla hiyo kwa niaba ya Waziri Jafo, unaakisi dhamira ya Serikali katika kushirikiana na sekta binafsi nchini katika kuchochea uchumi na maendeleo.

“Ni furaha kwangu kushuhudia hafla hii ya Uzinduzi wa Mradi wa Uunganishwaji wa Wajasiriamali Wadogo na Fursa za Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) na kwamba hatua hiyo ni matunda ya juhudi za ushirikiano zilizoanza mwaka jana tuliposaini Mkataba wa Usirikiano kati ya CRDB Foundation na UNDP.

“Tanzania ikiwa ni sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na mshiriki wa Eneo Huru la Afrika, ina fursa kubwa ya kunufaika na Soko la Afrika (AfCFTA) lenye watu zaidi ya bilioni 1.4. Biashara huria inaamisha kupanuka kwa masoko, kuongezeka kwa ajira, na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa wajasiriamali nchini.

“Programu hii tunayoizindua rasmi leo, kwa ushirikiano na UNDP, imejikita katika kuwezesha vijana na wanawake wajasiriamali ili washiriki kikamilifu katika Soko la Pamoja la Afrika, malengo ya mradi huu ni manne, ikiwa ni pamoja na; Kuahinisha na kutambua wajasiriamali wadogo na wa kati wa Kitanzania wenye uwezo wa kushiriki fursa za kibiashara za AfCFTA.

“Lengo la pili ni Kukusanya Taarifa muhimu kuhusu wajasiriamali hao, ikiwa ni pamoja na bidhaa zao, uwezo wao wa kuzalisha, uzoefu wao wa biashara, changamoto na matarajio yao, huku lengo la tatu likiwa ni Kuanzisha Mfumo wa Taarifa na Kanzidata ya Ujasiriamali kwa kusaidia juhudi za kuwajengea uwezo na kuwaunganisha na fursa mbalimbali,” alisema Mwambapa.

Mbele ya Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara, Mwambapa akalitaja lengo la nne la Mradi wa Uunganishwaji wa Wajasiriamali Wadogo wa Tanzania na Fursa za AfCFTA, kuwa ni Kupima Utayari wa Wajasiriamali wa Kitanzania wa kushiriki na kuwawezesha katika Soko Huria la Afrika.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, Shigeki Komatsubara, alikiri kufurahishwa na aina ya ushirikiano baina ya UNDP na CRDB Foundation, na kwamba ili kukua kiuchumi kwa mtu mmoja na taifa kwa ujumla, nguvu za wadau, Serikali na taasisi binafsi zinapaswa kuelekezwa kwa makundi ya wajasiriamali.

“Tanzania kama taifa, linahitaji sana nguvu ya wajasiriamali wanawake na vijana, uwekezaji na uwezeshaji wa aina yoyote kwa makundi hayo ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii. Inawapa wanawake na vijana nguvu na uhuru kifedha wa kufanikisha ndoto na malengo yao kibiashara, ikiwemo kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Haya ndio makundi vinara katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwa wingi ambazo ndio mahitaji ya msingi ya kila siku ya walaji na hata wazalishaji wakubwa, ndio maana sisi UNDP, hatusiti kuunga mkono juhudi zozote za kuyajengea uelewa, kuyawezesha na kuyafungulia fursa makundi hayo ya wanawake na vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *