HOSPITALI YA MLOGANZILA YAZIDI KUJIZATITI KATIKA UPANDIKIZAJI WA FIGO NCHINI

NA VICTOR MASANGU

Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila imeendelea kujikita katika kutoa huduma za ubingwa bobezi ambapo leo imewaruhusu wagonjwa watano na kufikisha idadi ya wagonjwa waliofanyiwa upandikizaji kufikia 15 tangu huduma hiyo ilipoanzishwa hospitali hapo mwaka 2023.

Akiongea na Waandishi wa habari wakati wa kuwaruhusu wagonjwa hao kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Naibu Mkurugenzi Mtendaji MNH-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema kutolewa kwa huduma hizo ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Magandi ameongeza kuwa hakuna sababu ya Watanzania kwenda nje ya nchi kwa huduma za upandikizaji figo kwakuwa wataalam wa ndani wana uwezo wa kutoa huduma hizo kwani wana weledi wa kutosha, miundombinu wezeshi, vifaa tiba na mazingira mazuri ya kutolea huduma.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo MNH Mloganzila Dkt. Immaculate Goima amesema hospitali hiyo ina wagonjwa takribani 90 ambao wanapatiwa huduma za kusafisha damu, ambapo kati ya hao 60 wanahitaji upandikizaji figo lakini hawajapata wa kuwachangia hivyo amewashauri ndugu zao kujitokeza kufanya vipimo na kuwachangia ndugu zao figo ili kuwaondolea changamoto wanazopitia.

Naye, Daktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo Dkt. Hamis Isaka amesema teknolojia iliyotumika kuvuna figo ni ya kisasa ya kutumia matundu madogo (Hand Assisted Laparoscopic Donor Nephrectomy) ambapo mtoa figo anakaa hospitalini siku mbili hadi tatu na kurudi katika majukumu yake kati ya wiki mbili hadi nne.

Mmoja wa wanufaika wa huduma hiyo amewashukuru wataalam wa hospitali hiyo kwa huduma nzuri za matibabu, ushauri, upendo na ufuatiliaji uliokuwa ukifanywa na wataalam hao kabla na baada ya kupandikizwa figo ambapo kwao imewapa faraja kubwa sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *