CRDB: Tupo Mtaani Kwako kukuletea Mfumo wa Malipo wa Lipa Hapa


NA MWANDISHI WETU

BENKI ya CRDB, imezindua Kampeni iitwayo Tupo Mtaani Kwako, inayolenga kuwarahisishia wateja wao kutumia Mfumo wa Malipo wa Lipa Hapa, ili kuwawezesha wateja wao kujiwekea urahisi wa kupata mikopo kutokana na mtiririko wa taarifa zao za mauzo kuonekana moja kwa moja kwenye mifumo ya benki hiyo.

Kampeni hiyo itakayodumu kwa miezi miwili, imezinduliwa Ijumaa Februari 7 kwenye Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambako Afisa Uendeshaji Mkuu wa CRDB, Bruce Mwile, aliwataka wafanyabiashara kote nchini kutumia mfumo wa Lipa Hapa, ili kuweka hai taarifa za mzunguko wa kifedha na kuwawezesha kukidhi vigezo vya kuomba na kupata mikopo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwile alisema CRDB imeenendelea kuwa mstari wa mbele katika kubuni bidhaa rafiki kwa jamii, inayojumuisha makundi yote kuanzia watoto, vijana, wanawake, wanaume na wazee, wafanyabiashara na wajasiriamali, lengo likiwa ni kuamsha ari ya kukua kwao kiuchumi.

Alibainisha kuwa mtandao mpana wa matawi zaidi ya 263 na mifumo ya kisasa ya kidijitali, unawapa uhakika wa kumfikia kila mhitaji wa huduma iwe matawini, kimtandao na hata kwenye ndege na kwamba mawakala zaidi ya 30,000 walionao, wanathibitisha dhamira ya benki hiyo katika kumsikiliza na kumpa suluhishi za kifedha kila Mtanzania.

“Nia ya mifumo yote hiyo ya kidijitali na mingine, ndio iliyotusukuma leo kuja kuzindua Kampeni ya Tupo Mtaani Kwako hapa Sokoni Kariakoo, mahali ambapo wafanyabiashara na wateja wao wana uhitaji mkubwa wa mifumo rafiki, sahihi na salama ya malipo katika kuchachua ukuaji wao kiuchumi na kibiashara.

“Kwa hakika Lipa Hapa imekuja kuleta mapinduzi makubwa katika mifumo ya malipo kidijitali na kumpa fursa mteja wetu kuingia katika rekodi za mzunguko wa pesa zake ili kumuwezesha kukidhi matakwa ya kukopa na kunufaika na mikopo yetu na huduma nyinginezo,” alisema Mwile katika hafla hiyo.

Naye Mkuu wa Idara ya Huduma za Mawakala wa Benki ya CRDB, Catherine Rutenge, alisema Huduma ya Lipa Hapa imekuja kuleta suluhu kwa wafanyabiashara na wanacnchi pale wanapotaka kufanya malipo ya huduma mbalimbali na kwamba kampeni hiyo inasadifu dira ya nchi, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Wananchi wote kupitia QR Code zetu za CRDB, wanaweza kufanya malipo kutoka kwenye waleti zao, akaunti zao, benki nyingine au mitandao ya simu, hata wasipokuwa na akaunti ya CRDB, wataweza kufanya malipo haya kupitia Namba za Lipa Hapa za CRDB, huduma ambayo haina malipo.

“Ni nyepesi kutumia, rahisi, ya haraka, na iliyo na usalama. Huduma hii inakwenda mbali kabisa ambapo sasa wa wafanyabiashara kwa kupitia taarifa za mfumo huu, tutaweza kukusanya rekodi zao kwa ajili ya kutumika kukopesheka, hasa ukizingatia wengi wao sio watunzaji wazuri wa taarifa zao,” alisema Rutenge.

Naye, Deogratius Mayenga, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Jumuiya ya Wanyabiashara wa Karikoo (JWK), alisema wamehudhuria uzinduzi huo kuwakilisha kundi kubwa la wafanyabiashara wa eneo hilo, ambalo ni kitovu cha biashara ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kwamba wamevutiwa na ubunifu uliozaa kampeni hiyo.

“Tunaishukuru sana CRDB kwa kutuletea huduma hizi za Lipa Hapa, ambayo inaenda kuleta urahisi kwa ufanyaji biashara ambao unakabiliwa na changamoto za maswali mengi ya wateja juu ya mifumo ya ulipaji wanayoweza kuitumia kutulipa tunapouza bidhaa zetu.

“Tunajua zipo huduma za Lipa Namba za mitandao ama taasisi nyingine za kifedha, lakini gharama zao ziko juu kwa kila muamala utakaopitia katika mifumo yao, lakini CRDB wao wanaitoa bure, zaidi wanaitumia kukusanya taarifa na rekodi za kifedha za mfanyabiashara ili kumpa fursa ya kunufaika na mikopo,” alisema Mayenga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *