Zitto Kabwe: Tundu Lisu karibu kwenye Mapambano ya Kidemokrasia

Dar es Salaam, Tanzania

KIONGOZI Mstaafu cha Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amekipongeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kufanikisha mchakato wa Mkutano Mkuu na Uchaguzi Mkuu, huku akimpongeza Mwenyekiti Mteule, Tundu Lisu na kumkaribisha katika mapambano ya Kidemokrasia.

Zitto Kabwe ambaye ni mwanachama wa zamani wa CHADEMA, ametumia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) kukipongeza chama hicho na viongozi wakuu wateule ambao ni Mwenyekiti Lisu na Makamu Mwenyekiti John Heche, huku akiahidi uongozi wa chama chake utawashika mkono na kuwaongoza.

“Nawapongeza CHADEMA kwa kuendesha Mkutano Mkuu wa chama chao na Uchaguzi Mkuu kupata viongozi wapya. Nawapongeza kaka yangu Tundu Lisu kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti na mdogo wangu John Heche kwa kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.

“Hakika tunawakaribisha katika uwanja wa mapambano ya kidemokrasia. ACT Wazalendo tumewatangulia kupanga safu (ya uongozi). Tutawashika mkono na kuwaongoza. Tunajenga taifa na nchi moja,” ameandika Zitto Kabwe mapema leo Jumatano Januari 22, baada ya kutoka kwa matokeo ya uchaguzi wa jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *