DAR ES SALAAM, TANZANIA
SAA chache baada ya Freeman Mbowe kumpongeza Tundu Lisu kwa kushinda uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Kiongozi Mstaafu cha Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amemkaribisha Mbowe katika ustaafu na maisha nje ya siasa za uongozi.
Zitto Kabwe, ambaye ni mwanachama na kiongozi wa zamani wa CHADEMA, ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kutoa ukaribisho huo kwa Mbowe, sambamba na kumpongeza kwa ushindani alioutoa katika mchakato huo na mchango wake mkubwa katika siasa za mageuzi Tanzania.

“Nakupongeza ndugu Freeman Mbowe kwa ushindani ulioutoa katika mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo. Nakupongeza zaidi wewe binafsi kwa mchango wako mkubwa katika Siasa za Mageuzi za Tanzania na chama chenu.
“Nakukaribisha Mwenyekiti Mstaatu Mbowe katika Ustaafu na kukuhakikiShia kuwa, kuna mengi nje ya Siasa za Uongozi katika kazi kubwa iliyo mbele yetu ya kujenga na kustawisha Demokrasia ya nchi yetu, ambayo inatuhitaji wana mageuzi walio ndani na nje ya uongozi,” amebainisha Zitto.