Tundu Lisu: Mbowe ameifanya CHADEMA kuwa kubwa kuliko vyama vyote

DAR ES SALAAM, TANZANIA

MWENYEKITI Mteule wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lisu, amempongeza mtangulizi wake Freeman Mbowe kwa utumishi uliotukuka, uliokipa hadhi ya kuwa Chama Kikuu cha Upinzani Bungeni kwa miaka 10, zaidi ni kukifanya kuwa Chama cha Siasa Kikubwa Zaidi Tanzania.

Tundu Lisu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 22, baada ya kutangazwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu, alikoshinda cheo cha Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa kwa kupata kura 513 dhidi ya 482 za Mbowe, aliyeongoza chama hicho kwa miaka 20 kati ya 30 ya chama hicho.

“Hili nilitaka kulisema baadaye, ila kwa sababu ukimaliza hotuba yako umesema unaondoka, wacha niseme sasa. Mwenyekiti wetu umeongoza CHADEMA kwa miaka yote kama inavyoeleweka kuwa ni Mwenyekiti aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi.

“Watangulizi wake walikaa madarakani kwa kipindi kimoja kimoja cha miaka mitano mitano, wewe umeongoza vipindi vinne vya miaka mitano mitano kila kimoja. Mwenyekiti wetu alipochukua hiki chama, kilikuwa na wabunge watano tu, lakini amekipeleka hadi kikawa Chama Kikuu cha Upinzani.

“Kikaenda na kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa miaka 10, amekifanya CHADEMA kuwa chama kikubwa, kuzidi vyama vyote vya Siasa nchini, kiasi kwamba hauwezi kukilinganisha na chama chochote.

“Kwa hiyo Mwenyekiti amekiongoza chama kuwa kikubwa katika historia ya nchi yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, historia ya chama hiki itapoandikwa wakati mimi na wewe tukiwa hatupo duniani, hautachwa kutajwa mchango wako, tunakushuru sana,” alibainisha Tundu Lissu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *