Ongezeko la joto lavunja rekodi ya Dunia

Na Irene Mark

WAKATI Tanzania ikirekodi ongezeko la juu la joto hadi nyuzi joto 0.7 mwaka 2024 imeelezwa kwamba joto la Dunia lilifikia nyuzi joto 1.55 kipindi hicho.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a amesema hayo leo Januari 22, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.

Dk. Chang’a amesema mwaka 2024 umevunja rekodi ya Dunia kwa kuwa na joto kali zaidi huku akibainisha kwamba hayo ni matokeo ya mabadiliko hasi ya tabianchi.

“TMA tutaendelea kushirikiana nanyi wanahabari ndio maana tunawashirikisha kwenye maandalizi ya msimu wa mvua za masika kama hivi.

“…Ushirikiano huu umetuongezea tija sisi Mamlaka na kuongeza uelewa na urahisi wa wananchi kupata taarifa sahihi za hali ya hewa kwa wakati, tunawashukuru na kuahidi kuendeleza ushirika huu,” amesisitiza Dk. Chang’a.

Aidha ameeleza namna Serikali inavyoendelea kuboresha ufanisi wa TMA kwa kuwezesha ujenzi wa rada mbili mwaka 2024 kwenye mikoa ya Mbeya na Kigoma na kumpeleka mafunzoni wataalam mbalimbali wa hali ya hewa.

“Mamlaka yetu ina jumla ya wafanyakazi 560 kati yao 80 sawa na asilimia 15 ya watumishi wote wapo masomoni ndani na nje ya nchi wakiongeza ujuzi hasa matumizi ya teknolojia.

“Kwa uwekezaji huu unatupa fursa wa kuendelea kuwa kitovu cha ubora katika masuala ya hali ya hewa Afrika, sababu za kuwa hivyo tunazo kivifaa na rasilimali watu,” amesema Dk. Chang’a.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi huyo, wataalam wawili wa TMA wapo nchini Burundi ili kuwajengea uwezo wataalam wa hali ya hewa wa nchi hiyo.

“Serikali ya Burundi imeomba kwetu tuwape wataalam ili kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa wa nchini kwao na sisi kwa kuwa tonayo hazina ya kutosha tumewatuma wabobezi wetu huko.

“Hii maana yake sisi tumebobea kwenye sekta ya hali ya hewa na tumekuwa mfano wa kuigwa Afrika Mashariki na Kati kwa taarifa sahihi, bora na zinazotoka kwa wakati,” amejinasibu Dk. Chang’a.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *