Mbowe awaagiza Lisu, Heche kuunda Tume ya Upatanishi kutibu Majeraha ya Uchaguzi

Dar es Salaam, Tanzania

MWENYEKITI Mstaafu wa Chadema, Freeman Mbowe, ameutaka uongozi mpya wa chama hicho chini ya Mwenyekiti Mteule Tundu Lisu na Makamu Mwenyekiti John Heche, kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa kufuata Katiba, pamoja na kuunda Tume ya Upatanishi ili kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi.

Mbowe ameyasema hayo leo Jumatano Januari 22 wakati wa hotuba yake ya mwisho, baada ya kushindwa Uchaguzi Mkuu wa nafasi ya Mwenyekiti alikopata kura 482 dhidi ya kura 513 alizopata mshindi wa nafasi hiyo Tundu Lisu, huku Odero Charles Odero akiambulia kura moja tu.

“Tumefanya uchaguzi huru na wa haki, na hili halipaswi kuwa tukio la mara moja, linapaswa kuwa la mchakato wote unaojenga nchi. Nimesema mara nyingi na leo nasema tena, kwa namna ambavyo wagombea mbalimbali na mashabiki wao walivyojinasibu katika kampeni, imeiachia CHADEMA majeraha makubwa.

“Na hili jambo wana CHADEMA tusipolikubali na kulitibu, tutaumiza ‘brand’ ya chama chetu, ambayo tunatakiwa wote kuiponya. Na kwa maana hiyo basi, nilisema na nasema tena hapa, tumemaliza uchaguzi leo kwa kumshukuru Mungu kuwa tumewapata viongozi wapya,

“Lakini ambacho ni kweli na tunapaswa tukiseme, ni kwamba uchaguzi huu umeacha majeraha mengi ndani mwetu. Ushauri wangu kwa viongozi wetu mlioingia madarakani, kakiponyeni chama chetu. Mimi niliahidi kama ningeshinda uchaguzi huu, ningeunda tume ya ukweli na upatanishi.

“(Kupitia tume hiyo) Watu wakazungumze yaliyojiri kuelekea uchaguzi huu, pale watu walipokoseana adabu, walipovunja nidhamu, walipokosa maadili, walipokibagaza chama chetu, wakasameheane na kupeana mikono ili CHADEMA yetu iwe ‘stronger’ zaidi.

“Nawaasa sasa kama ‘Baba wa Chama’ (makofi mengi), sina hakika niwaase au niwaagize (wajumbe wanajibu kwa pamoja; “waagize”). Kama mnaniheshimu, kama mtu ambaye mnatambua kazi niliyoifanya kwenye chama hiki, basi nawaagiza; haraka undeni Tume ya Ukweli na Upatanishi, katibuni majeraha ili muweze kujenga umoja.

“Nilisema jana na narudia leo, ushindi wa yeyote katika chama hiki ni ushindi wa chama. Asitokee mmoja wenu akatawaliwa na kiburi cha ushindi, oneni ulazima tena wa haraka wa kutibu majeraha. Hapa kuna watu wamepondeka mioyo, sio kwamba hatukubali matokeo, lakini tunakubaliana kwamba tumekanyagana.

“Hilo jambo karekebisheni ili sura na sifa ya chama chetu ikaendelee kuwa nzuri sio tu kwa wanachama wetu, bali hata kwa nyie katika uongozi wenu, mkawe na uongozi wenye furaha na amani na watu wengine, usiokuwa na visasi. Kumbukeni salamu yetu ya ‘No Hate, No Fear,” alisisitiza Freeman Mbowe.

Katika suala zima la kuheshimu Katiba na Demokrasia, Mbowe alisema: “Tembeeni katika Katiba ya Chama, msitembee katika mapenzi yenu au hisia zenu binafsi, tembeeni kwenye Katiba ya Chama. Wakati wote jengeni chama hiki kupitia Katiba.

“Pale ambapo mtafikiri kwenye Katiba kuna upungufu, shirikisheni wengine, fuateni taratibu za kidemokrasia, rekebisheni Katiba mjenge taasisi. Wakati mnyukano umepambana moto, wapo watu waliniambia Mheshimiwa Mbowe toka tutakuadhiri, nikasema nitafia kwenye Demokrasia.

“Kwahiyo nashukuru Demokrasia niliyoijenga, imesema na tutahitaji Dekomrasia hiyo iendelee kusema kwa wengine katika chama hiki na hata walio nje wajifunze kutoka kwetu,” alibainisha Mbowe ambaye alikuwa akishangiliwa mno na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema, akaongeza:

“Wote lengo letu la kuijenga Demokrasia katika nchi hii haliwezi kufifishwa na uchaguzi, nashukuru tumeonesha demokrasia kwa vitendo, naondoka nikiwa na roho nyeupe sana. Naondoka nikiwa ‘very proud’ kwa kazi kubwa na nzuri niliyoifanya kwa zaidi ya miaka 30 katika chama.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *