NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BENKI ya CRDB, imetunukiwa tuzo mbili za Kimataifa, ikitambuliwa kuwa Mwajiri Kinara Zaidi Tanzania ‘Top Employer 2025,’ kutoka Taasisi ya Top Employers Institute, zinazothibitisha kuwa benki hiyo ni Kitovu cha Ubora, lakini pia zikiakisi jitihada za CRDB katika kuboresha mazingira ya kufanya kazi.
Tuzo hizo kutoka Top Employers Institute ya Uholanzi, zinatambua jitihada kubwa za CRDB katika kuweka mazingira bora ya kazi, inayowekeza kwenye vipaji na mafunzo, ujumuishi na usawa wa kijinsia, sambamba na kutoa fursa kwa wafanyakazi wake kukua kiutendaji na kuchochea mabadiliko chanya.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa, wakati wa utambulisho wa tuzo hiyo kwa vyombo vya habari, hafla iliyofanyika Makao Makuu ya CRDB, ikihudhuriwa pia na Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Wafanyakazi wa benki hiyo, Timothy Fasha.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Rutasingwa alisema sio rahisi kwa CRDB kutambuliwa na Top Employers kama Mwajiri Kinara Zaidi Tanzania, kwani wabobebu hao wa masuala ya ajira, ustawi wa wafanyakazi na rasilimali watu hufanya ukaguzi, tafiti na mchujo ili kupata vinara wenye sifa.
“Tuzo hii ni ‘reflection’ ya jitihada zote ambazo tumekuwa tukizifanya kama benki katika kuboresha mazingira ya wafanya kazi kutekeleza majukumu yao, ni ishara ya wazi kwamba CRDB inajali na kuthamini wafanyakazi wake kwa kuwajengea mazingira wezeshi ya kuharakisha mafanikio yao binafsi na ya kitaaluma.
“Kupata tuzo hii sio kitu rahisi, Top Employers Institute ni taasisi bobevu inayofanya kazi kwa weredi mkubwa, ikiwemo kuzingatia vigezo na masharti, kupitia kaguzi za kina ili kuona usahihi wa mazingira bora ya kufanyia kazi katika sehemu zao za kazi.

“Inakagua kuona namna tunavyowalinda na kuwajali wafanyakazi na familia zao kuhakikisha wote wanakuwa kwenye ustawi, namna tunavyochochea vipaji vyao na kuleta matokeo bora kwa biashara yetu, lakini zaidi ni kuwa Top Employers hawatosheki tu na maelezo yetu, bali hujikita katika kufanyia ukaguzi na utafiti kujiridhisha.
“Na kote huko, CRDB tumepata alama za juu za ukaguzi na leo tuko hapa kuwaambia Watanzania kuwa tuzo hizi ni kielezo tosha cha dhamira yetu ya kuboresha hali za wafanyakazi kwa kiwango cha juu, kwa kuwekeza katika maslahi na ustawi wa wafanyakazi wetu.
“Hii inathibitisha kuwa mafanikio ya benki yanatokana na uwepo wa wafanyakazi wenye afya, wenye ari na uwezo wa kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wetu kwa mustakabali wa ustawi na ukuaji wa benki yetu,” alisisitiza Rutasingwa huku akiwashukuru wafanyakazi kwa bidii na kujitolea kwao
Aliongeza ya kwamba, hiyo sio tuzo ya kwanza kwa CRDB, kwani mwaka jana 2024 ilipata zaidi ya tuzo 50, ikiwemo tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), na kwamba hilo linathibitisha namna benki yake ilivyo na ‘consistency’ katika kuwa kinara wa kile wanachokifanya.
Rutasingwa alifafanua kuwa, kuweza kushinda tuzo hiyo, taasisi mbalimbali ukaguliwa katika maeneo nyeti, ikiwemo mkakati wa usimamizi na maendeleo ya wafanyakazi, upatikanaji na usimamizi wa vipaji, huduma za ustawi, utofauti na ujumuishwaji, mazingira rafiki ya kazi na usawa wa kijinsia mahali pa kazi.
