NA MWANDISHI WETU, DAR
NAIBU Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk. Doto Biteko, amesema uenyeji mwenza wa Tanzania katika kuandaa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Nyota wa Ndani (CHAN 2025) na Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), ni kielezo na uthibitisho wa ukuaji wa Diplomasia iliyojengwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hayo ameyasema leo Jumatano Januari 15, wakati akifungua Kongamano la Kujadili Fursa Zitokanazo na Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali hizo za baadaye mwaka huu na zile za mwaka 2027, ambapo alisema fursa hizo hazitamnufaisha tu Mtanzania mmoja mmoja, bali taifa kwa ujumla.
“Nchi yetu imepata heshima kubwa ya kimataifa, ambayo haijaja kwa bahati mbaya au kwa kubahatisha. Hii ni fursa iliyotokana na ukuaji wa Diplomasia iliyojengwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake, baina yetu kama nchi na mataifa mbalimbali duniani.
“Leo hii hapa tunajadili fursa zitokanazo na uenyeji wa CHAN 2025 na AFCON 2027, lakini kuna matukio na mikutano mingi mikubwa ya kimataifa iliyofanyika na itakayofanyika Tanzania, ndio maana nasisitiza kuwa washiriki jipangeni vema sio tu kujadili fursa hizo, bali kuzifanyia kazi wakati wa mashindano hayo.
“Kwa kuwa ni mashindano makubwa, yatakayokusanya wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani, tukiwa wenyeji tunao wajibu wa kuhakikisha tunakuwa na maandalizi sahihi,
kama wenyeji tuna haki za msingi kuhakikisha tunanufaika na mashindano hayo kupitia nyanja za usafirishaji, malazi, burudani na utalii.
“Manufaa au fursa zitakazokuja kutokana na mashindano haya, hazitamnufaisha tu Mtanzania mmoja mmoja, bali zitachochea na kukuza uchumi wetu kama taifa,” alisisitiza Dk. Biteko wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo lililoshirikisha mamia ya wadau wa michezo, hususan soka.
