Kesi ya Dk. Slaa yakwama baada ya kutofikishwa mahakamani, sasa kusikilizwa Jan. 17

HATMA ya Dhamana ya Kesi ya Jinai Namba 993 ya Mwaka 2025, inayomkabili aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CAHDEMA, Dk. Wilbroad Slaa, imekwama kwa mara nyingine, hii ni baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kushindwa kusikiliza, baada ya mshtakiwa kutofikishwa mahakamani hapo leo Januari 13.

Dk. Slaa (76), alifikishwa mahakamani hapo Januari 10, akikabiliwa na kesi ya kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X (zamani Twitter), akidaiwa kutenda kosa hilo chini ya Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao Namba 14 ya Mwaka 2015, kosa alilodaiwa kutenda Januari 9, 2025.

Dk. Slaa alifikishwa mahakamani hapo Januari 10, 2025 akikabiliwa na kesi hiyo, ambapo alitarajiwa kufikishwa tena mahakamani hapo leo kwa ajili ya kujua hatma ya dhamana yake baada ya Upande wa Jamhuri kuwasilisha kiapo cha kuzuia dhamana.

Katika kesi hiyo inayovuta hisia za wadadisi na wachambuzi wa masuala ya siasa Kitaifa na kimataifa, Dk. Slaa anatetewa na Mawakili sita, wakiongozwa na Biniface Mwabukusi, Peter Madeleka na Hekima Mwasipu, huku Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili Tawabu Issa.

Wakili wa Serikali, Issa alisema kuwa kesi hiyo imeitishwa leo kwa ajili ya mjadala wa dhamana, lakini mtuhumiwa hajafika mahakamani, ambapo
Wakili wa utetezi, Madeleka kwa niaba ya timu ya utetezi, alisema Jamhuri ndio walimfikisha Dk. Silaa mahakamani na kuzuia dhamana yake, hivyo kupelekwa mahabusu kwa amri ya mahakama.

Wakili huyo alibainisha kwamba mahakama ndio ilisema aletwe leo, ambapo Jamhuri yenyewe haijui yupo wapi, na kutaka waliotakiwa kumleta mteja wao mahakamani, wachukuliwe hatua za kisheria maana haijulikani mtuhumiwa kama amekufa ama lah na kuomba kesi isikikizwe bila mtuhumiwa kuwepo.

Kutokana na mvutano wa kutofikishwa mahakamani kwa mtuhumiwa na hatma ya dhamana yake, huku hoja nyingine zikiibuka kutoka pande zote mbili za Mawakili wa Serikali na Utetezi, Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *