
Afisa wa UTT AMIS, Dorice Mlenge, akitoa elimu juu ya Uwekezaji kwa wastaafu watarajiwa wa Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (Tanesco) – Mkoa wa Tanga wakati wa semina iliyofanyika jijini humo.

NA MWANDISHI WETU, TANGA
KAMPUNI ya Uwekezaji ya UTT AMIS, imeendesha semina ya siku mbili kwa wastaafu watarajiwa wa Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (Tanesco) – Mkoa wa Tanga na kuwaonesha fursa za uwekezaji kupitia mifuko mbalimbali, ikiwemo Mfuko wa Uwekezaji wa Umoja, Wekeza Maisha, Mfuko wa Watoto, Mfuko wa Kujikimu, Mfuko wa Ukwasi (Liquid Fund) na Hatifungani (Bond Fund).
Akizungumza wakati wa semina hiyo iliyofanyika Januari 9 na 10, afisa wa UTT AMIS, Doris Mlenge, alisema semina hiyo kwa wafanyakazi wanaojiandaa kustaafu, ililenga kuwapa elimu ya namna sahihi ya kutumia pesa zao za mafao na kuwaonesha fursa za uwekezaji na hatari ya kuzitumia kufanya biashara wasizo na uzoefu nazo.
“Lengo ni kuwahimiza wasifanye biashara ambazo hawakuwahi kuzifanya, waepuke biashara zile ambazo hawana uzoefu nazo, kwani ni hatari kwao na pesa zao, lakini pia tumezungumza nao juu ya umuhimu wa kutawanya pesa zao za mafao katika uwezekzaji mbalimbali unaopatikana kwetu UTT AMIS.
“Kwa maana kwamba, kwa mfano wakiwekeza katika ‘Bond Fund’ ya UTT AMIS, watakuwa wakipata gawio la kila mwezi, ambalo litawasaidia kuendesha maisha yao kama wafanyavyo wafanyabiashara kupitia faida zao, ambapo mtu akiweka Sh. Mil. 10 na kuendelea, tunampa faida ya kila mwezi na ile pensheni yake, maisha yake yanaenda vema.
“Pia kupitia kusanyiko hili, tumezungumzia Uwekezaji kwa Watoto na Wafanyabiashara, kwa sababu kuna wastaafu waliobobea katika biashara pia, kwa maana zile biashara wanazofanya huku wakiendelea kufanya kazi kama waajiriwa, ili wajenge mazingira ya uwekezaji utakaosaidia kukuza pato lao,” alisema Mlenge.
Akiwanoa wafanyakazi na wastaafu hao watarajiwa, mlenfe alisema Liquid Fund ni uwekezaji unaoanzia Sh. 100,000 na kuendelea, ambapo mwekezaji anaweza kutoa muda wowote utakapo na kwamba mfuko huo unapiga hesabu ya ulichokiweka kila siku, faida yake inakuza mtaji wa mwekezaji mmoja mmoja ama vikundi.
“Yaani ukiwekeza Sh. 100,000 kwa mfano, mfuko ukatengeneza faida ya Sh. 1,000 kwa mwezi, ile Sh. 1,000 inajiongeza katika mtaji wako, ndio kusema faida inajiongeza katika fedha zako za uwekezaji iwe wa mtu mmoja ama vikundi mbalimbali vya kijamii.
“Pia kuna hii Bond Fund, ni mfuko ambao walengwa wake wakuu ni wastaafu, ambao wengi pesa zao wakishazipata kwa mkupuo mmoja, ndani ya miezi sita zimeisha. Pia, pesa ya wastaafu hupotea mara kwa mara miongoni mwa wastaafu kwa sababu wanalazimika kufanya biashara au kitu ambacho hawakuwa na uzoefu nacho,” alibainisha Mlenge.