UTT AMIS: Wastaafu fanyeni uwekezaji kwa ustawi wa maisha baada ya ajira

NA MWANDISHI WETU, TANGA

KAMPUNI ya Uwekezaji ya UTT AMIS, imetambulisha fursa ilizonazo kwa Wafanyakazi Wanaojiandaa Kustaafu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) – Mkoa wa Tanga, walioshiriki semina iliyoandaliwa na Mstaafu Forum, Taasisi Bobevu ya Mafunzo ya Uwekezaji na Maandalizi ya Kustaafu.

Semina hiyo ya siku moja, ilifanyika Januari 10 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Hospitali ya Bombo jijini hapa, ambapo Afisa wa UTT AMIS, Ester Kahabi alitoa mada, kuzungumza na wastaafu hao watarajia, kuwapa elimu ya namna sahihi ya kuwekeza pesa zao za mafao na hatari ya kufanya biashara wasizo na uzoefu nazo.

Katika semina hiyo, Kahabi aliitaja baadhi ya Mifuko ya Uwekezaji kuwa ni pamoja na Mfuko wa Uwekezaji wa Hatifungani (Bond Fund), Mfuko wa Uwekezaji wa Ukwasi (Liquid Fund), Mfuko wa Watoto (Watoto Fund), Mfuko wa Umoja (Umoja Fund), Mfuko wa Jikimu (Jikimu Fund) na mingineyo.

Kahabi alisema Liquid Fund ni mfuko wa uwekezaji unaoanzia Sh. 100,000 na kuendelea, ambapo mwekezaji anaweza kutoa muda wowote utakapo na kwamba faida yake inakuza mtaji wa mwekezaji mmoja mmoja ama vikundi, akitolea mfano kuwa ukiwekeza Sh. 100,000, mfuko ukatengeneza faida ya Sh. 1,000 kwa mwezi, ile Sh. 1,000 inajiongeza katika mtaji wako.

“Pia kuna hii Bond Fund, ni mfuko ambao walengwa wake wakuu ni wastaafu, ambao wengi pesa zao wakishazipata kwa mkupuo mmoja, katika muda mfupi zinaisha. Pia, kuna hii ya Watoto Fund, ambayo inajikita katika ujenzi wa kesho bora ya mtoto kielimu, kiafya na kiuchumi, hata pale mzazi atapokuwa nje ya mfumo rasmi wa ajira,” alibainisha Kahabi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *