MASAA machache kabla ya kupigwa kwa fainali ya Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup 2025), kati ya timu za Taifa za Zanzibar na Burkina Faso, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza zawadi ya Goli la Mama kwa Zanzibar Heroes iwapo itashinda na kutwaa taji.

Goli la Mama ni zawadi ya pesa taslimu kiasi cha Sh. Mil. 5 kwa kila bao linalofungwa na timu za Tanzania katika ushindi wa mechi za mashindano ya kimataifa na licha ya kutokuwepo kwa zawadi hiyo katika mechi za Mapinduzi Cup, Rais Samia jioni hii amewaahidi Zanzibar Heroes kulamba mkwanja iwapo watawachapa Burkina Faso.
“Ninaipongeza Zanzibar Heroes kwa kufanikiwa kufika hatua ya fainali ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi. Mmejitoa, mmejituma na sote tunajivunia safari yenu hadi sasa.
“Mchezo huu wa fainali ni nafasi ya kipekee kwenu kuandika historia, nasi tuko nyuma yenu kuwaunga mkono. Ninawatakia kila la kheri, na ninawaahidi katika mchezo huu wa fainali Goli la Mama litakuwepo,” imemaliza taarifa ya Rais Samia kwa Watanzania kuelekea fainali hiyo.
Zanzibar inaumana na Burkina Faso leo saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa Gombani, kisiwani Pemba, hii ni baada ya timu hizo kumaliza katika nafasi za juu za msimamo uliohusisha pia timu za Taifa za Kenya na Tanzania Bara. Burkina wamemaliza hatua hiyo wakiwa na alama Saba, moja juu ya Zanzibar Heroes.