CRDB yazindua Ada Loan, Mikopo na Makusanyo ya Ada sasa Mtelezo tu

NA MWANDISHI WETU, DAR

KATIKA kutatua changamoto za mkwamo wa kiuchumi mwanzoni mwa mwaka kwa wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo vilivyosajiliwa kwenye Mfumo wa Ada Fasta, Benki ya CRDB imezindua Huduma ya Ada Loan inayolenga kutoa mikopo ya ada na kuziwezesha shule na vyuo kukusanya ada kwa urahisi.

Uzinduzi wa Ada Loan umefanyika jijini Dar es Salaam leo Jumanne Januari 7, ambako Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, alisema huduma hiyo ni kielelezo cha dhamira ya benki yake katika kugusa maisha ya kila mmoja miongoni mwa wateja na Watanzania, ikiwemo utatuzi wa changamoto za kifedha.

“Tukiwa mwanzoni mwa mwaka, utekelezaji wa malengo ya mwaka 2025 yameanza rasmi na yanahitaji uwezeshaji, nasi CRDB kila siku tunalenga kugusa maisha ya kila mmoja miongoni mwa wateja na Watanzania kwa ujumla na kutatua matatizo ya kifedha.

“Tunapofika Januari kila mwaka, kila mmoja anakuwa ametoka kwenye matumizi makubwa ya Sikukuu za mwisho wa mwaka, ambapo mwanzo wa mwaka kila mmoja ana majukumu ya kulipa ada, kulipa kodi na kadhalika. Leo tuko hapa kuzindua suluhishi la changamoto tunazokumbana nazo tunapofika Januari, changamoto za uwezeshwaji kulipa ada.

“Wadau wetu katika Ada Loan sio tu wazazi na walezi, bali pia wamiliki wa shule, ambao wametupa mrejesho wa maboresho ya huduma yetu ya Ada Fasta, ndipo tukaja na suluhushi ya tatizo la wazazi walezi katika ulipaji wa ada za wanafunzi wao, lakini pia wamiliki wa shule kukusanya malipo ya ada kwa urahisi,” alisema Nshekanabo.

Alibainisha ya kuwa mzazi ama mlezi mwenye akaunti ya CRDB na Huduma ya Sim Banking, anaweza kukopa hadi Sh. Mil. 3 ambazo atazifanyia marejeshpo kwa kipindi cha miezi sita kwa riba ya asilimia 13, nia ikiwa ni kuwezesha wazazi, walezi kulipa kwa wepesi ada za wanafuniz ambao wangebaki nyumbani wakisubiri wazazi wajitafute.

“Leo hii tunazindua suluhisho hili ambalo kwa urahisi kabisa, mzazi mwenye akaunti CRDB au mfanyakazi au mfanyabiashara na amejiunga na Sim Banking, atapata huduma hii, ili mradi mtoto wake awe anasoma Shule ya Msingi, Sekondari au Vyuo, kinachotumia Mfumo wa Ada Fasta, basi anaweza kupata mkopo wa kulipa ada,” alisisitiza Nshekanabo.

Aliongeza ya kwamba hadi sasa wana shule za msingi, sekondari na vyuo takribani 1,000 vilivyojiunga na Mfumo wa Ada Fasta, huku akitoa wito kwa shule na vyuo ambavyo bado hawajajiunga, kufanya hivyo haraka kwani wakati ndio huu, kwani watasaidia shule na vyuo kufanya makusanyo ya ada za wanafunzi kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa CRDB, Stephen Adili, alisema Mikopo ya Ada kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari nchini, unaakisi dhamira ya benki yake katika kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wao, ikiwemo mikopo ya kukabiliana na changamoto za kifedha hasa katika kipindi hiki cha mwanzo wa mwaka wa masomo.

“CRDB ni benki kinara katika kuhakikisha tunawafikia na kuwapatia huduma rafiki popote walipo na kwa wakati. Tunao mfumo wa Ada Fasta, tukaona tuuongezee thamani kwa wamiliki wa shule na wazazi ama walezi, ndipo tukaja na bidhaa hii muhimu ya Ada Loan kurahisisha mifumo ya elimu na ulipaji ada kupitia mikopo.

“Ada Loan ni mrejesho kutoka kwenu na tunajivunia ushirikiano baina ya wawekezaji wa sekta ya elimu na CRDB, na tunaamini kupitia huduma hii mpya, changamoto zote za ulipaji na ukusanyaji wa ada kwa wanafunzi wa shule na vyuo, zinaenda kumalizwa na huduma hii mpya,” alisema Adili.

Naye Rais wa Chama cha Wawekezaji Binafsi Katika Sekta ya Elimu Tanzania, (TAPIE), Mahmod Mringo, alisema chama chake kinajisikia furaha kutokana na ujio wa Ada Loan ambao ni kama ushindi wa vita vilivyoanza tangu mwaka 2013, walipojaribu kuwasilisha pendekezo linaloainisha ukubwa wa tatizo la ulipaji ada kwa wazazi.

“Mwaka 2013 tukiwa katika Ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini Mbeya, tuliwasilisha pendekezo, na tangu hapo tukawasilisha katika Nyanja mbalimbali kuanzia ngazi ya chini, mkoa, taifa na hata bungeni, kuonesha ukubwa wa tatizo na changamoto tutazopitia wamiliki na wawekezaji katika masuala ya ada.

“Kwa furaha ya kipekee na hili acha niweke wazi, nilikuwa nasikia kaulimbiu ya CRDB Ni Benki Inayomsikiliza Mteja, nikadhani ni kauli tu, lakini tulipoweka mezani changamoto za ada, mwanzo walisita, lakini baadaye wakachukua hatua, tunashukuru leo sio stori tena juu ya hilo, ni mafanikio.

“Sisi ni wawekezaji tuliokopa, uwekezaji wetu katika sekta ya elimu hautokani na pesa tulizochimba kama dhahabu, hatuishi kwa kukopesha, sisi sio mabenki, lakini tunachopitia baina ya sisi na wazazi ama wanafunzi, ni changamoto kubwa, inayifikia hatua ya kuonekana kama nasi ni wakopeshaji, kitu ambacho sio sahihi,” alisema Mringo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *