Rais Samia aipongeza Yanga, aipa Mil. 15/- za ‘Bao la Mama’

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Young Africans ‘Yanga’ kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), akisema ushindi ukawe chachu ya kushinda mechi mbili zilizosalia na kufuzu hatua inayofuata.

Ikiwa nyumbani Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Yanga imeizabua TP Mazembe mabao 3-1, shukrani kwa Clement Mzize (mawili) na Stephanie Aziz Ki, ushindi uliofufua matumaini ya kikosi hicho kufuzu robo fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ngazi ya klabu Afrika.

Katika taarifa yake kwa umma, aliyoitoa baada ya filimbi ya mwisho, Rais Samia ambaye hulipa Sh. Mil. 5 kwa kila bao la ushindi wa michuano ya Klabu Afrika, amesema: “Hongera kwa Klabu ya Yanga kwa ushindi dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Nawatakia kila la kheri katika michezo iliyosalia kwenye mashindano haya. Endeleeni kutupa burudani na kufanya kazi njema ya kuipeperusha vyema bendera ya nchi yetu kimataifa,” amesema Rais Samia katika taarifa yake.

Kutokana na ushindi huo, Yanga imepewa kitita cha Sh. Mil. 15 za ‘Bao la Mama,’ zawadi anayotoa kwa kulipia Sh. Mil. 5 kwa kila bao katika mechi ya ushindi wa mechi za kimataifa, kitita ambacho kitaongezeka kuwa Sh. Mil. 10 kwa kila bao la hatua ya robo fainali na Mil. 20 kwa bao la nusu fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *