MATUMAINI ya Yanga kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2024/25), yamefufuliwa, baada ya ushindi mnono wa mabao 3-1 iliyopita dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), katika pambano la nne kwa klabu hizo kwenye Kundi A la michuano hiyo.
Yanga inayonolewa na Sead Ramovic, imelazimika kutoka nyuma kwa bao 1-0 lililofungwa na wageni mapema dakika ya 16 kwa mkwaju wa penalti uliopigwa na mlinda mlango wa Mazembe, Allioune Badara Faty, baada ya winga wake kuangushwa ndani ya boksi na beki wa kushoto, Chadrack Boka.
Clement Mzize akairudisha Yanga mchezoni baada ya kuisawazishia dakika ya 33 na pambano kwenda mapumziko kukiwa na sare ya bao 1-1, ingawa Yanga walitawala dakika zote na kutengeneza nafasi ambazo walishindwa kuzibadili kuwa mabao.
Kipindi cha pili, Stephanie Aziz Ki akaiongezea Yanga bao la pili dakika ya 56, kabla ya Mzize tena kuiandikia bao la tatu na la ushindi dakika ya 60, hivyo kuinasua timu mkiani mwa msimamo wa Kundi A, ilikofikisha pointi nne, sawa na walizonazo MC Alger ya Algeria, ambao wanacheza na Al Hilal ya Sudan.
Huu ni muendelezo wa ubora wa kikosi cha Yanga chini ya Mjerumani Sead Ramovic, ambayo tangu alipopoteza mechi mbili za kwanza za michuano hii, hajafungwa mchezo wowote, akishinda mechi nne za Ligi Kuu Tanzania, sare moja na ushindi huu mmoja dhidi ya Mazembe, ambao wameshushwa mkiani wakiwa na alama zao mbili baada ya sare mbili na vipigo viwili.
