Rais Samia amteua aliyekuwa Bosi DCEA, DC Moshi, kuwa Mkurugenzi NIDA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Bwana, James Wilbert Kaji, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, kabla ya uteuzi huo, Bwana Kaji alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Bwana Kaji anachukua nafasi iliyokuwa ikikaimiwa na Bwana Deusdedith Buberwa, katika kuiongoza Mamlaka hiyo muhimu ambayo inalalamikiwa na mamilioni ya Watanzania kutokana na mkwamo wa upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa.

Kaji, amaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), haijaelezwa ataapishwa lini, licha ya taarifa ya Balozi Kusiluka kusema uteuzi wake umeanza rasmi leo Desemba 18.

Nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi Iko wazi kwa sasa na uteuzi wa mbadala wake waweza kufanya na Rais Dk Samia muda wowote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *