Dar es Salaam – Kutokana na kuongezeka kwa visa vya kipindupindu katika mikoa ya Mwanza na Simiyu, Marekani inatoa msaada wa ziada wa TZS bilioni 1.18 (sawa na USD $500,000) kwa mikoa hii. Mpango huu ni mwendelezo wa msaada wa afya wa serikali ya Marekani kwa jamii zilizoathirika na milipuko ya kipindupindu nchini Tanzania.
Kupitia mradi wa Maji Safi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), Marekani imetoa TZS milioni 591 (USD $250,000) kwa kila moja ya mikoa ya Simiyu na Mwanza, na kutuma timu za kiufundi za maji, usafi wa mazingira, na usafi wa mikono kusaidia ofisi za afya za mikoa husika. Timu hizi, kwa kushirikiana na wadau wazawa, zinatoa vidonge vya kutakasa maji, kusafisha vyanzo vya maji, na kuendesha programu za uhamasishaji wa jamii ili kuzuia kuenea kwa kipindupindu.
“Hatua yetu ya haraka inaonyesha dhamira yetu ya kuokoa maisha na kupunguza kuenea kwa kipindupindu Tanzania,” alisema Kaimu Balozi Andrew Lentz. “Marekani itaendelea kuwa mshirika wa karibu katika kuimarisha mifumo ya afya ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na kukuza upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira—mambo muhimu katika kupambana na ugonjwa huu unaoweza kuzuilika.”
Mapema mwaka huu, Marekani ilitoa TZS milioni 473 (USD $200,000) kwa ufadhili wa dharura kusaidia juhudi za kuzuia na kukabiliana na kipindupindu kufuatia milipuko iliyokuwa imeathiri mikoa 18 kote Tanzania. Tangu Septemba 2023, visa vya kipindupindu vimeongezeka Tanzania, na kuripotiwa zaidi ya visa 2,200 na zaidi ya vifo 40. Serikali ya Marekani, kupitia USAID na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC), imeendelea kushirikiana kwa karibu na viongozi wa jamii za Tanzania kuongeza upatikanaji wa maji safi, kuwafundisha wafanyakazi wa afya ya jamii na wakazi kuhusu njia bora za kuzuia, na kusaidia harakati za haraka za timu za kukabiliana na mlipuko. CDC inatoa vidonge vya kutakasa maji kwa watu walio na VVU na kuongoza juhudi za kudhibiti katika vituo vinavyofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR). Msaada huu wa ziada utaimarisha uratibu, kuchochea rasilimali, na kuwezesha jamii zilizoathirika zaidi huko Simiyu na Mwanza kuzuia kuenea kwa kipindupindu na kuokoa maisha.
Msaada huu wa dharura wa TZS bilioni 118.19 (USD $50 milioni) ni sehemu ya ahadi ya Marekani ya kubadilisha miundombinu ya maji, usafi wa mazingira, na usafi wa mikono nchini Tanzania. Hadi sasa, zaidi ya Watanzania milioni mbili wamepata maji safi na huduma bora za usafi wa mazingira. Marekani inaendelea kuunga mkono juhudi za kupanua upatikanaji wa maji safi na mifumo bora ya maji taka kama msingi wa maisha yenye afya na ustawi kwa Watanzania wote.
