BAADA ya msoto wa muda mrefu, hatimaye ‘Mwana Mfalme’ Prince Mpumelelo Dube, amefungua akaunti ya mabao katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, baada ya leo kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao matatu ‘hat trick’ msimu huu na kuipa Yanga ushindi wa 3-2 dhidi ya Mashujaa FC ya Kigoma.

Dube aliyetwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi hiyo (MoTM), aliitanguliza Yanga mapema dakika ya saba, Kisha kufunga bao la pili dakika ya 21 na kuipeleka Yanga mapumziko ikiwa mbele kwa bao 2-1, hii ni baada ya David Ulomi kuwafungia Mashujaa FC bao kunako dakika ya 45 ya mchezo huo.
Katika kipindi cha pili, Dube alithibitisha ‘ufufuko’ wake kwa kuifungia Yanga bao la tatu dakika ya 53, kabla ya Idrisa Stambuli kuwapa Mashujaa bao la pili dakika ya 62, bao lililodhihirisha kuwa huenda ‘ufufuko’ ni wa Dube pekee, lakini Yanga bado iko kwenye kiwango kile kile kilichowapa vipigo vinne katika mechi sita zilizopita za ndani na kimataifa.
Kwa ushindi huo, Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania, wamepanda kwa nafasi moja kutoka ya nne hadi ya tatu, waiwa na pointi 30, sawa na walizonazo Singida Black Stars waliocheza mechi 14.
Azam FC ambao waliocheza mechi 15, wanaongoza msimamo huo wakiwa na alama 33, mbili juu ya Simba wenye pointi 31 na michezo 12, sawa na waliyocheza Yanga. Mashujaa FC wamebaki nafasi ya saba wakiwa na pointi 19 baada ya kushuka dimbani mara 14.
