Jaji Mkuu: Mawakili someni vema Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, amewataka mawakili wapya wa kujitegemea waliosajiliwa wakiwemo Majaji, Wasajili wa Mahakama Kuu, Mahakimu na Maofisa wengine wa Mahakama, kuisoma vema Rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili kujua uelekeo wa taifa katika Robo ya Pili ya Karne ya 21.

Prof. Ibrahim ametoa wito huo Desemba 12, wakati wa kupokelewa, kusajiliwa na kuapishwa kwa mawakili 524 wa kujitegemea ambapo Wanawake walikuwa 228 na Wanaume 296, katika Sherehe za 71 tangu mwaka 1986, sherehe zilizofanyika kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali na wadau wa Sekta ya Sheria.

Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, imezinduliwa hivi karibuni na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ikilenga kugusa moja kwa moja maboresho ya maisha ya watu, elimu, afya, ustawi wa amani na haki, pamoja na kuwa na Dira Jumuishi itakayomshirikisha kila mwananchi kuchangia Maendeleo ya Taifa.

“Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, imezinduliwa jana, ninyi ambao mtafanyakazi katika hiyo Robo ya Pili ya Karne ya 21, hiki ndio kielezo chenu cha Mabadiliko ya Elimu ya Sheria ambayo Tanzania inayatarajia.

“Kwa sababu msiposoma ile dira, hamtojua mwelekeo taifa katika Robo ya Pili itavyokwenda, hutojua mazingira ambayo utatolea huduma ya sheria, kwahiyo nawasihi sana, sana, hata katika hayo Mabadiliko ya Elimu ya Sheria, Mheshimiwa Rais wa TLS na wadau wa Mnyororo wa Sheria, mnapaswa kuisoma vema hiyo dira.

“Tunapaswa kujiuliza, Elimu ya Sheria tuliyonayo itafaa kutekeleza dira hiyo au tunahitaji uwezo mwingine, ujuzi mwingine ambao utasaidia katika safari hiyo ya 2050,”? alihoji Jaji Mkuu na kusisitiza umuhimu wa kuisoma na kuielewa kwa kina, sambamba na kuitolea maoni na mitazamo.

“Je, vyuo vikuu, Shule ya Sheria kwa Vitendo, inawatayarisha vya kutosha mawakili ambao wataweza kufanya kazi kwa weledi na ufanisi katika Robo ya Pili ya Karne ya 21, ni lazima tujiulize kwamba elimu tuliyopata, inatuwezesha sisi kuwa na uwezo wa kiushindani wa kupata ajira katika Robo ya Pili ya Karne ya 21?

“Kwahiyo, huu ni mtihani wako (Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika – TLS), katika miaka yako mitatu ya uongozi wako, hakikisha unashirikiana vema na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sekta zote za sheria zikiwemo Mahakama, tujiulize je tuendelee kufundisha sheria kama tulivyofundisha katika Karne ya 20?

“Je tunaweza kushindana nje ya mipaka ya Tanzania kupata ajira katika Sekta ya Sheria? Tunaweza kushindana na mawakili kutoka mataifa mengine duniani? Hayo ndio maswali ambayo tunapaswa kujiuliza,” alisisitiza Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim, huku akiwataka mawakili kujivunia uwezo na sio vyeti vyao vya Elimu ya Sheria.

Aliwaambia ya kwamba, nguzo kuu ya kupitia kufikia kilele cha kuitwa Wakili Mwenye Weledi ni Uwezo wa Kutafsiri Sheria na kutoa Huduma Bora za Kisheria kwa Jamii, hasa baada ya kupitia Chuo Kikuu, Shule Kuu ya Sheria kwa Vitendo, pamoja na kupitia katika mikono ya Wanasheria Wazoefu na kuona namna sheria inavyofanya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *