MWENENDO WA KIMBUNGA “CHIDO” KATIKA BAHARI YA HINDI


Dar es Salaam, Tanzania
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa
kimbunga “CHIDO” katika Bahari ya Hindi.


Kati ya siku ya jana Alhamisi tarehe 12 na leo Ijumaa tarehe 13 Disemba, 2024, Kimbunga
“CHIDO” kimeendelea kusalia katika eneo la bahari kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar
huku kikiendelea kuashiria kuelekea katika maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji katika kipindi
cha siku tatu zijazo (tarehe 14 hadi 16 ya mwezi Disemba, 2024).


Aidha, kimbunga hicho bado hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja
hapa nchini. Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO”
kinatarajiwa kupita (kaskazini mwa Msumbiji) na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo
uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya mkoa wa
Mtwara na maeneo jirani hususan kwa siku ya tarehe 15 Disemba 2024.

Vilevile, upo uwezekano wa kutokea matukio ya upepo mkali wa bahari unaofika kilomita 40
kwa saa na mawimbi makubwa yanayofika mita 2 katika maeneo ya mwambao wote wa pwani
ya nchi yetu hasa kwa siku ya tarehe 15 Disemba, 2024.


USHAURI: Watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla wanashauriwa kuendelea
kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga
“CHIDO” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa
kila inapobidi.
Imetolewa na:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *