Chuo Kikuu Mzumbe, Kuhne Foundation ‘wawapiga msasa’ Maafisa Manunuzi, Ugavi

NA MWA NDISHI WETU

CHUO Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam na Taasisi ya Kuhne Foundation Tanzania, wameendesha Semina kwa Maafisa Manunuzi na Ugavi kutoka Taasisi za Umma, Binafsi, Vyuo Vikuu, Wahitimu na Vijana walio kwenye Mafunzo kwa Vitendo, iliyolenga kuwaongezea utambuzi na uelewa wa Sheria Mpya ya Manunuzi ya Mwaka 2023.

Semina hiyo ambayo ni zao la ushirikiano baina ya Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam na Kuhne Foundation, imefanyika kwa siku tatu ikishirikisha Maafisa Manunuzi, Ugavi na Wahitimu 40, walionolewa na Alfred Sallwa, ambaye ni Mkufunzi wa Masuala ya Ununuzi Katika Sekta ya Umma na Mnyororo wa Thamani wa Ugavi na Usambazaji.

Akizungumza katika hafla ya kufunga Semina na kukabidhi vyeti kwa washiriki hao, Sallwa alisema Semina hiyo iliandaliwa na Ndaki ya Dar es Salaam ya Chuo Kikuu Mzumbe na kudhaminiwa na Kuhne Foundation, lengo likiwa ni kutoa elimu endelevu inayohusiana na Mabadiliko ya Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma iliyoanza kutumika Juni mwaka huu.

“Sheria hii ni mpya, imeanza kutumika mwaka huu Juni, kwa hiyo mabadiliko haya kuna maeneo yameongezewa nguvu, kama vile katika Utawala wa Sheria, Uwajibikaji wa Wahusika Katika Manunuzi, sanjari na Sheria ya Mienendo ya Kimaadili, kwa maana kuna Makatazo Maalum yametolewa ambayo Sheria ya Ununzi imetaja.

“Lakini pia adhabu husika pale ambapo Sheria ya Manunuzi ya Umma imeenda ndivyo sivyo na kimsingi semina hii ilikuwa jukwaa muhimu kwa Maafisa Manunuzi kutoka taasisi mbalimbali, vijana waliohitimu vyuo katika sekta hiyo, ambapo ‘wameji-update’ kutokana na mabadiliko hayo.

“Zilikuwa siku tatu za wao kujifunza Sheria Mpya ya Manunuzi, kujua changamoto zilizosababisha mabadiliko na kujua namna ya kuiendea Sheria Mpya ili kulinda maadili na miendeno ya Utumishi wa Umma na Ununuzi. Kwa waliohitimu vyuo, semina hii imekuwa msaada kwao kujua fursa zilizopo katika sheria mpya,” alisema.

Alibainisha ya kwamba, wamejifunza juu ya Sheria Mpya namna inavyohimiza utengaji na matumizi sahihi ya asilimia 30 ya utoaji zabuni kwa makundi maalum, yanayohusisha wanawake, vijana na walemavu, na kwamba kwao ilikuwa ni fursa, wamejifunza na kulijua hilo namna ya kuliendea.

Aidha, alisisitiza ya kwamba Semina hiyo imewaongezea kitu kikubwa wahitimu na wale walio kwenye mafunzo kwa vitendo ‘internship program’ katika kujua sheria mpya, kwa sababu kazi wanazotafuta na kuziomba watapitia usaili ambao sehemu ya mchujo wake utahusisha weledi na ujuzi wa Sheria Katika Manunuzi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Ushirikiano huo, Profesa Omary Swalehe wa Chuo Kikuu Mzumbe, alisema kupitia ushirikian huo, kuna shughuli mbalimbali zinazofanywa na kwamba semina hizo za kitaaluma ni miongoni mwa hizo shughuli za kiushirikiano.

“Kwa hiyo seimna hii ni namna ya kupitia Sheria Mpya ya Manunuzi ya Umma na Kanuni zake. Tumekuwa hapa tangu Jumatano, Alhamisi na leo Ijumaa, lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wataalamu wetu wa Sekta ya Manunuzi na Ugavi, hasa maafisa walio kwenye Taasisi za Umma nchini.

“Hii yote ni katika kuwawezesha kujua sheria na kanuni zipi zimebadilika na zipi zinaendelea kutumika na zina athari gani kwa ujumla wake,” alisema na kuongeza: “Kupitia ushirikiano huu wa Mzumbe na Kuhne Foundation, tumekuwa tukipata mrejesho na hivi karibuni tutafanya mapitio ya jumla kupata maoni ya washiriki.”

Alibainisha ya kuwa, tayari mdhamini wao Kuhne Foundation ameshatenga fedha za kufanikisha hilo na Februari mwakani watafanya mapitio ya jumla ya kupata mrejesho wa Mawazo kutoka kwa washiriki wa semina mbalimbali zilizokuja kupitia ushirikiano huo.

“Kwa Watanzania, wito wangu kwao ni kuchangamkia semina kama hizi zinapotokea, ambazo hawalipi chochote kwani zinakuwa zimeshalipiwa na mdhamini, huku akiwapongeza washiriki 40 walioshiriki mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti, huku akiwataka kuwa mabalozi wema katika sekta hiyo ya kimkakati.

Naye Mathew Erick Mkoma, kutoka Kuhne Foundation Tanzania, alisema mizizi ya taasisi yake hiyo isiyokuwa ya Kiserikali, ni nchini Ujerumani na Uholanzi na kwamba inajihusisha zaidi na utoaji elimu vyuoni, lengo likiwa ni kuwafikia na kuwaongezea uwezo na uwelewa walioko vyuoni katika mnyororo wa thamani wa ugavi na ununuzi.

“Lengo la semina hizi ni kuondoa yale makando kando yanayouzunguka Mnyororo wa Thamani wa Manunuzi na Ugavi kwa Sekta za Umma, ndio maana tunatoa nafasi na kusisitiza kuzitumia fursa kama hizi, ili kujiongezea elimu itakayomsaidia mshiriki katika nafasi yake sehemu yake ya kazi.

“Tunatamani elimu hii iwaendee na kuwafikia wengi zaidi, waweze kuboresha utoaji huduma wao mahali pa kazi ndio maana tumekuwa na semina aendelevu za mara kwa mara, huku tukitoa miito ya Watanzania hususani walioko kwenye Sekta ya Umma, kujitokeza na kuzitumia kwa ustawi wa taasisi zao na taifa kwa ujumla,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *