TMA: Kimbunga CHIDO kitapita Mtwara

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwepo wa kimbunga “CHIDO”
katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.

Mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kinatarajiwa kuelekea maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji kuanzia Desemba 13 hadi 16, 2024.

“Kwa sasa, kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini… hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo kimbunga “CHIDO”
kinatarajiwa kupita pia maeneo ya kusini mwa nchi yetu.

“Upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa itakayoambatana na upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya Mtwara na maeneo jirani hususan kati ya Desemba 14 na 16, 2024,” ilisomeka sehemu ya taarifa iliyotolewa na TMA.

Mamlaka hiyo imewashauri watumiaji wa bahari na wananchi kwa ujumla kuendelea
kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na kutoa taarifa zake kila wakati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *