WAZIRI mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, ameanza kazi mara moja baada ya uapisho wake, ambapo amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini, huku akiahidi kutenga muda wa kukutana na Idara, Vitengo, Vyombo Vya Usalama na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo.
Akizungumza alipotembelea Ofisi za Idara ya Uhamiaji Zanzibar na kuongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Maduhu Kazi, Waziri Bashungwa amesema lengo la awali ni kukutana na Idara, vitengo na vyombo vya usalama ni ili kupata taarifa ya utendaji kazi, mafanikio pamoja na changamoto, ili kuweka mikakati ya kuzifanyia kazi.

Aidha, ziara hiyo iliyofanyika punde baada kuapishwa katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar leo Jumanne Novemba 10, ilihudhuriwa pia Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa Vyombo Vya Usalama vilivyopo Chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, pamoja na Watumishi wa Umma wa Wizara hiyo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Bashungwa alisema: “Nitapata fursa ya kukaa na ninyi kuangalia katika majukumu, mnafanikiwa wapi, changamoto ziko wapi, jitihada zinazoendelea katika utatuzi wa changamoto na tufanyeje ili tuweze kushirikiana kutatua hizo changamoto.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Sillo, alimkaribisha Waziri Bashungwa na kueleza kuwa Dira ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni kuwa wizara ambayo itaifanya nchi kuwa na amani, utulivu na mahali ambapo sheria zinaheshimika.
Mheshimiwa Sillo ameeleza dhamira ya Wizara ni kulinda maisha na mali, kuwezesha na kudhibiti utokaji na uingiaji nchini kwa raia na wageni, kuwarekebisha wafungwa na kutoa huduma kwa wakimbizi waliopo nchini.
