Yanga kunani palee.!! Imefia dakika zilezile za Al Hilal

KATIKA Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Mabingwa Watetezi Yanga walikumbana na vipigo viwili mfululizo, wakianza na Azam FC (1-0), kisha Tabora United (mabao 3-1). Wakamtimua Miguel Gamondi na kumtangaza Sead Ramovic ‘Germany Machine’ kama Kocha Mkuu.

Baada ya hapo, Yanga ikaangukia pua lipowaalika Al Hilal ya Sudan katika mechi ya kwanza Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2024/25), ambayo ilikuwa ni mechi ya tatu mfululizo kwenye mashindano yote, ikiwa ni ya kwanza kwa ‘Germany Machine.’

Ufufuko walioupatia Ruangwa mkoani Lindi dhidi ya Namungo FC katika Ligi Kuu Tanzania, haukuwa na maana kuwa wamerejea ubora wao, badala yake jana imethibitika kuwa ‘furaha ya maskini haidumu.’

Wakiwa ugenini mjini Algiers nchini Algeria, usiku wa jana Yanga wamekumbana na kipigo cha nne katika mechi 5 zilizopita kwenye mashindano yote.

Mabao 2-0 kutoka kwa wenyeji wao MC Alger katika Kundi A la CAF CL 2024/25, ni kipigo cha pili baada ya kile cha Al Hilal nyumbani Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam wiki jana.

Maswali yamekuwa mengi kwa ‘wenye timu yao.’

Kuna wanaomnyooshea kidole kocha mpya Sead Ramovic, wakidai ameelemewa na ukubwa wa nyota kikosini, wengine wakisema hana mbinu timu inachezaji kienyeji, wapo wanaosema amekosa ‘creativity’ katika mpango kazi wake ‘game plan,’ hajui kuutandika mkeka ‘kamari’ ya mabadiliko ‘sub.’

Hapa hakosi watetezi, wanaomtetea wanamficha kwenye kivuli cha ugeni wake kikosini, huku lawama zao wakizielekeza kwa wachezaji, ambao sio jambo la ajabu kucheza dakika 90 bila kuwa na ‘on target’ angalau moja. Hii inafikirisha na kuzua maswali mengi.

Injinia Hersi Ally Said, anaweza kuwa ndiye kiongozi aliyenwagiwa sifa sana Yanga katika kipindi cha takribani miaka mitano hii, lakini naye ameanza kulaumiwa.

Anatajwa na mashabiki na hata wadadisi wa masuala ya ‘football’ ya Afrika kama ndiye ‘mkandarasi’ aliyejenga msingi imara wa matokeo haya mabovu yanayovunwa sasa na timu yake.

Kwamba alipaswa kutumia IQ kubwa baada ya vipigo viwili katika Ligi ‘kuyajenga’ na ‘mzee mwenzake’ Gamondi, kuliko kuiongoza Kamati Tendaji kujadili na hatimaye kuvunja mkataba wa Gamondi.

Kama aliridhia maazimio ya kumuondoa Gamondi wiki mbili tu kabla ya kuanza kwa mechi za Hatua ya Makundi CAF CL, sasa anakwepaje lawama hizi kwa mfano..?

Daaaahhh, maswali na vidole vya lawama ni vingi. Hoja za Nguvu na Nguvu za Hoja zinajengwa juu ya hilo, tafakuri tunduizi zinamwagika kwenye magroup ya WhatsApp ya mashabiki wa timu, mitandaoni na vijiweni.

Lakini kama ujuavyo, hoja na tafakuri za ovyo nazo zipo, zimejaa tu huko. Haji Manara anatajwa sana huko, Mzee Magoma naye yumo.

Manara na Magoma (ambao hawana ushirikiano) wanatajwa kama wabobezi wa propaganda zinazoweza kuwa zinaitafuna Yanga, wengine wanashauri warudishwe kundini kutoka ‘vichakani’ waliko, kila mmoja akijiona hatendewi haki na uongozi.

Kama uliangalia ‘game’ ya jana, Yanga imefia kwenye dakika zile zile ilizofia Benjamin Mkapa ilipoumana na Al Hilal na hili ndio swali kuu nalojiuliza, ilikuwaje Yanga vs Al Hilal na kisha MC Alger vs Yanga, dakika za mabao zikalingana hivi..?

Jijini Dar es Salaam, dakika 45 za kwanza ziliisha kwa sare tasa, kisha Adama Coulibaly kuitanguliza Al Hilal dakika ya 64, kabla ya Yasir Mozamil kupigilia msumari dakika ya 90+…

Imekuwa tena hivyo jana usiku, Ayoub Abdellaoui alipoitanguliza MC Alger dakika ya 64 na Soufiane Beyazid kudidimiza jahazi la Yanga dakika zile zile za jioooooooni (90+)

Yanga, kunani paleee
Mbona kila kitu pale kimekufaaa…??

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *