NA MWANDISHI WETU
BENKI ya CRDB imezindua Hatifungani ya Miundombinu ya Samia ‘Samia Infrastructure Bond,’ ikilenga kukusanya Sh. Bilioni 150 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kimkakati ya miundombinu nchini, ili kutanua mtandao wa usafiri na Sekta ya Usafirishaji wa Barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA).
Hatifungani hiyo imezinduliwa Novemba 29 na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, aliyemwakilisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, sambamba na ufunguzi wa maombi ya uwekezaji, ambapo Rais Samia aliahidi uwekezaji wa Sh. Milioni 200, ambapo ahadi za jumla zilikuwa takribani Sh. Bilioni 37 kutoka kwa taasisi na watu binafsi.

Makamu wa Rais, Dk. Mpango aliahidi uwekezaji wa Sh. Milioni 100 katika uzinduzi huo, ulioenda sambamba na ufunguzi wa dirisha la mauzo ya Hatifungani hiyo, yatakayofanyika kwa siku 50 hadi Januari 17 mwakani, itakapoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) baada ya dirisha kufungwa.
Ukiondoa ahadi za Rais Samia (Milioni 200), Dk. Mpango (Milioni 100), baadhi ya taasisi zilizoahidi kufanya uwekezaji kupitia Hatifungani ya Samia na thamani ya ahadi zao kwenye mabano ni; NSSF (Bil. 10), PSSSF (Bil. 10), UTT Amis (Bil. 1), Bodi ya Mfuko wa Barabara (Sh. Bil. 1.5) na STAMICO (Sh. Bil. 1.
Kianzio cha manunuzi ya Samia Infrastructure Bond ni Sh. 500,000 na kuendelea, ambapo mwekezaji atavuna riba ya asilimia 12 kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano, huku gawio kwa mwaka likiwa ni mara 4 na hakuna makato ya kodi na baada ya miaka mitano, kila mwekezaji atarudishiwa pesa yake.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema benki yake inatambua na kuthamini jitihada za Rais Samia katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu nchini na wao kama taasisi ya fedha wanajiona wanao haki na wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo.

“Leo hii tunazindua Hatifungani ya Miundombinu ya Samia, lakini huu sio mwanzo, CRDB ni benki ya kizalendo iliyoshiriki miradi mingi mikubwa na ya kimkakati, ikiwemo ujenzi wa ‘terminal 3’ ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Reli ya Kisasa (SGR) na usambazaji umeme vijijini (REA).

“Aidha, Mheshimiwa Mgeni Rasmi, wakandarasi ni watu muhimu sana, lakini kwetu sisi CRDB, wakandarasi wazawa ni muhimu zaidi na ndio maana tumejikita katika kunyanyua uwezo wa wakandarasi wetu katika maeneo kadhaa, ikiwemo kuwapa mitaji ya uwekezaji, mitaji ya kuendesha shughuli zao na mengineyo.
“Kwenye soko la fedha nchini, ukwasi umeendelea kuwa changamoto na hasa pale wawekezaji wa pesa kwenye mabenki wanapokuwa wachache. Sisi CRDB tumejikita katika kutafuta mitaji yenye masharti nafuu ili tuemdelee kukuza uchumi wa nchi hii kwa kusaidia wawekezaji katika sekta mbalimbali,” alisema Nsekela.
Alibainisha kuwa dhamira hiyo ndio inayowasukuma kutafuta wadau ndani na nje ya nchi ambao wanashirikiana nao kwa kutambua maslahi na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya Rais Samia na wasaidizi wake, walioigeuza Tanzania kuwa sehemu inayovutia kila mtu kufanya uwekezaji.

Makamu wa Rais, Dk. Mpango aliishukuru CRDB sio tu kwav kubuni na kuja na Hatifungani ya Miundombinu ya Samia, bali kumwalika Rais Samia mwenyewe kushiriki uzinduzi huo, ambao unaakisi dhamira ya kweli ya benki hiyo katika kusapoti jitihada za ujenzi na maboresho ya miundombinu nchini.
“Rais alitamani kuwa nanyi hapa, lakini msongo wa majukumu alionao ukamsukuma kunituma kumwakilisha hapa. Rais anawashukuru kwa heshima kubwa mliyopa ya kuwa mgeni rasmi na pia kutumia jina lake katika Hatifungani hii ya kihistoria inayoakisi jitihada zake kujenga ubia wa Serikali na Sekta Binafsi.
“Matumaini ya Rais Samia ni kuwa, Hatifungani hii itakuza na kuchochea mwitikio wa taasisi zingine kutumia chanzo hiki cha fedha katika kusaidia na kufadhili miradi ya maendeleo, ndio maana anaahidi Serikali yake itaendelea kushirikiana na CRDB na taasisi zingine za fedha katika kutatua changamoto za maendeleo,” alisema.

Alibainisha kuwa Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ili kuchochea maendeleo na hivyo kuongezeka kwa mtandao wa barabara nchini kutoka kilomita 13,235 mwaka 2020, hadi kufikia kilomita 15,366 mwaka huu wa 2024, sambamba na ongezeko la bajeti ya TARURA.
“Bajeti ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini, imeongezeka kutoka Bil. 414.45 mwaka 2019/20 hadi kufikia Sh. Bil. 841.2 mwaka 2024/25. Hata hivyo mahitaji ya Barabara mijini na vijijini ni makubwa, kwa kuzingatia ukubwa wa nchi, mahitaji ya kukuza Uchumi, kuboresha huduma za jamii na ongezeko kubwa la idadi ya watu.
“TARURA inakabiliwa na uhitaji wa Rasilimali fedha ili kuweza kuwalipa wakandarasi kwa wakati. Fedha kutoka serikalini na mapato ya ndani ya TARURA, hakika hazitoshi ndio maana tunaipongeza CRDB kwa Hatifungani hii ambayo inalenga kuongeza uwezo wa TARURA kuongeza mtandoa wa Barabara zake,” aliongeza.
