SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mchango mkubwa na kuwa chachu ya kuiwezesha timu ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).

Tanzania imefuzu fainali hizo za mwakani nchini Morocco baada ya juzi kuichapa Guinea kwa bao 1-0 la Saimon Happygod Msuva, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambako Rais Samia alilipia viingilio na kuruhusu Watanzania kuingia bure dimbani hapo ili kuisapoti timu.
Baada ya ushindi huo, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ilisema Rais Samia ametoa kitita cha Sh. Milioni 700 za kuwazawadia wachezaji na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Hemed Suleiman ‘Morocco,’ yakiwa matukio mawili ya karibu yanayoakisi mchango Rais Samia.
Kwa mujibu wa taarifa ya TFF iliyosainiwa na Afisa Habari wake Clifford Ndimbo, Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia, amemshukuru na kusema uwezeshaji, hamasa na mchango wa Rais Samia, umekuwa msaada mkubwa na chachu ya mafanikio ya Taifa Stars.
“Mheshimiwa Rais Samia amekuwa na mchango mkubwa katika mpira wa miguu na hamasa yake siku zote imekuwa chachu ya timu zetu za Taifa kufanya vizuri, ikiwemo hata upande wanngazi ya klabu. Wote nu mashuhuda wa ushiriki wake wa karibu ulivyotuwezesha kufuzu AFCON 2025 nchini Morocco mwakani,” amesema Karia.
Aidha, Rais Karia amewashukuru wachezaji wa Taifa Stars na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya na kufanikisha kufuzu fainali hizo, huku pia akiwashukuru mashabiki, Watanzania, wadau na vyombo vya habari nchini kwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo.
