Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
Uwekezaji ni moja ya njia bora za kujenga mustakabali wa kifedha wa mtu binafsi au jamii kwa ujumla.
Kwa miaka zaidi ya 20, Kampuni ya Uwekezaji wa Pamoja ya UTT AMIS imejidhihirisha kuwa chombo madhubuti cha kusaidia wawekezaji kufikia malengo yao ya kifedha.
Kupitia mifuko yake, ikiwemo Umoja Fund, Wekeza Maisha, Jikimu, Liquid Fund, na Bond Fund, UTT AMIS inatoa fursa za kipekee kwa wananchi wa Tanzania kuwekeza fedha zao kwa usalama, ufanisi, na faida ya muda mrefu.

Mifuko hii imeonyesha mafanikio makubwa, kama ilivyoainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa UTT AMIS, Simon Migangala, wakati wa mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam kabla ya Mkutano Mkuu wa Wawekezaji wa Mfuko wa Umoja (Umoja Fund).
Akieleza, Migangala amesema kuwa thamani ya mifuko hiyo imeongezeka kutoka Sh Trilioni 1.5354 mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2023, hadi kufikia Shilingi Trilioni 2.2382 mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024. Hii ni sawa na ongezeko la Shilingi Bilioni 702.8, linaloashiria ukuaji wa asilimia 45.7.
Ongezeko hilo halikupatikana kwa bahati bali ni matokeo ya usimamizi thabiti wa uwekezaji, ongezeko la idadi ya wawekezaji, na hali nzuri ya soko la mitaji.
Migangala amebainisha kuwa mwaka 2024 pekee, idadi ya wawekezaji imeongezeka kwa asilimia 32, ambapo wawekezaji wapya 79,519 walijiunga na mifuko hiyo, ikilinganishwa na wawekezaji 47,480 waliojiunga mwaka uliopita, ongezeko la asilimia 24.
“Mifuko yote imeendelea kutoa faida nzuri kwa wawekezaji wake. Kwa mfano, faida ya Mfuko wa Umoja ilikuwa asilimia 12.1,” alisema Migangala, akisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa malengo ya muda mrefu.
Migangala pia alieleza kuwa mafanikio haya ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa kampuni hiyo uliomalizika Juni 30, 2024.
Mpango huo uliolenga kukuza thamani ya mifuko umezidi matarajio. Alisema kuwa thamani ya mifuko ilikadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 1,007.9 ifikapo Juni 2024, lakini imepita matarajio hayo na kufikia Shilingi Trilioni 2.2. “Hii ni mara mbili ya kiwango tulichokitarajia,” alisema, akifafanua kuwa juhudi za kuboresha mifumo ya uwekezaji na huduma kwa wawekezaji zimechangia mafanikio haya makubwa.
Migangala amesisitiza kuwa UTT AMIS itaendelea kuimarisha mifumo yake ya kisasa na kuibua bidhaa mpya ili kufanikisha lengo la kuhakikisha wawekezaji wanapata huduma bora na faida nzuri zaidi. “Katika kipindi cha mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango mpya, tunatarajia kukamilisha maboresho ya mifumo yetu kama msingi wa kukuza biashara yetu,” aliongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya UTT AMIS, Profesa Faustine Kamuzora, amesema kuwa kwa zaidi ya miongo miwili ya uwepo wa kampuni hiyo, mafanikio yake yanaendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kifedha kwa wawekezaji. “Ni furaha kuona wawekezaji wenzangu wakifaidi matunda ya uwekezaji wa pamoja kwa njia tulivu (passive investment), ambayo inatoa faida hata wakati tukiendelea na shughuli nyingine za kimaisha,” alisema Profesa Kamuzora.
Amewapongeza wawekezaji wote kwa imani yao kwa UTT AMIS na uamuzi wa busara wa kuwekeza katika mifuko hiyo. Alibainisha kuwa kupitia uwekezaji huo, wawekezaji wengi wameweza kugawana faida kubwa na kuboresha maisha yao.
“Fedha nyingi zimetengenezwa na kugawiwa kwa wawekezaji kwa kipindi chote cha uwepo wa UTT AMIS. Hii ni ishara ya kuaminika kwa mifuko yetu na fursa zinazotolewa na kampuni yetu,” aliongeza.
Kwa ujumla, mafanikio ya UTT AMIS si tu yanahimiza umuhimu wa uwekezaji wa pamoja bali pia yanaonyesha jinsi taasisi hiyo inavyoweka misingi ya kuwawezesha wawekezaji wa kitanzania kufikia malengo yao ya kifedha kwa njia bora, salama, na endelevu.