Mawaziri 10 washiriki kuaga miili ya waliokufa ghorofa Kariakoo

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameongoza idadi kubwa ya Mawaziri, Manaibu Waziri na Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuaga miili ya watu 16 waliofariki baada ya kuangukiwa ghorofa eneo la Kariakoo.

Miili ya marehemu hao imeagwa na maelfu ya wakazi wa Jijini Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja leo Jumatatu Novemba 18, ambako Waziri Mkuu Majaliwa alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, aliyepo nchini Brazil, alikoalikwa kushiriki Mkutano wa G20.

Simanzi na vilio vilitawala tukio hilo, lakini gumzo likiwa idadi kubwa ya Mawaziri, Manaibu Mawaziri na Makatibu Wakuu na viongozi mbalimbali waandamizi wa serikali zote mbili, wote wakiongozwa na Waziri Mkuu Majaliwa aliyeongozana na mwenyeji wao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Baadhi ya Mawaziri walioshiriki hafla hiyo na Wizara zao kwenye mabano ni William Lukuvi (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu), Hamza Hassan Jumaa (Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar) na Jennister Mhagama (Waziri wa Afya).

Wengine ni pamoja na Suleiman Jafo (Waziri wa Viwanda na Biashara), Mhandisi Hamadi Masauni (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi), Abdallah Ulega (Waziri wa Mifugo na Uvuvi), huku Manaibu Mawaziri wakiwa ni Zainabu Katimba (Naibu Waziri Nchi, TAMISEMI) na Daniel Sillo (Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi).

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Dk. Salum Seif Salum (Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar), Ally Gugu (Katibu Mkuu wa Mambo ya Ndani ya Nchi) na Mohammed Abdullah (Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari).

Wengine ni Grace Maghembe Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Logatius Mativila, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Abbas Mtemvu (Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Idd Azzan Zungu (Mbunge Ilala – Naibu Spika wa Bunge la Tanzania na Amon Mpanju (Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *