Maelfu ya waombolezaji wamiminika Mnazi Mmoja kuaga waliokufa Kariakoo

SAA moja kabla ya kuanza kwa shughuli za kuaga miili 13 ya watu waliokufa baada ya kuporomokewa na jengo la ghorofa nne Kariakoo jijini Dar es Salaam, maelfu ya waombolezaji wamejitokeza katika Viwanja vya Mnazi Mmoja hivi sasa. 

Jengo la ghorofa nne lililokuwa makutano ya mitaa ya Kongo na Mchikichi, liliporomoka juzi Novemba 16 saa 3 asubuhi na kusababisha vifo vya watu 13 kwa takwimu zilizotangazwa Jana Novemba 17, na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, huku wengine zaidi ya 80 wakijerihiwa nankupatiwa matibabu kwenye Hospitali za Muhimbili, Amana na Mnazi Mmoja.

Idadi ya watu hapa imekuwa ikiongezeka na tayari viti vilivyotengwa na mahema yaliyowekwa yamejaa na watu kwa sasa wanalowana mvua nyepesi inayoendelea kunyesha hapa, ingawa hadi sasa majeneza yenye miili ya marehemu hao haijawasili hapa 

Huenda umati ukaongezeka zaidi viwanjani hapa, kwani watu wengi kwa sasa wako Hopsitali ya Amana kuzitambua maiti hizo, Kisha baada ya hapo ndipo maiti zitaketwa mahali hapa kwa hafla ya kuwaaga na kukabidhiwa kwa ndugu zao, tayari kwa maziko kulingana na Imani za kila mmoja wao. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajia kuongoza shughuli zote za kuaga miili ya marehemu, huku viongozi mbalimbali wa ngazi za Mkoa na Wilaya wakitarajia kuungana na waombolezaji hawa. 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila anatarajia kuwa miongoni mwa viongozi hao, sambamba na wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, Kamati za Ulinzi Mkoa na Wilaya, Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *